NADHARIA NA UHAKIKI WA USHAIRI
Jina la kitabu – MALENGA WAPYA
Waandishi – TAKILUKI
Wachapishaji – OUP
Utangulizi
Malenga wapya ni kitabu kinachozungumzia masuala mbalimbali ya kijamii kama vile ukombozi wa mwanamke, umuhimu wa Kilimo,
umuhimu wa kutatua matatizo katika jamii, umuhimu wa kutenda mema, matumizi mazuri ya pesa pamoja na athari za ukoloni mamboleo.
Maudhui
Dhamiri kuu: Ukombozi
Katika diwani hii msanii amejadili dhamira ya ukombozi wa kiuchumi, kisiasa, kitamaduni na kifikra.
Ukombozi wa Kiuchumi
Katika kujadili ukombozi wa kichumi msanii amesisitiza mambo muhimu yafuatayo:
Kwanza, Umuhimu, wa kuinua uchumi wetu. Katika suala la kuinua uchumi wa nchi yetu wasanii wanasema kuwa kuna umuhimu wa kujenga uchumi imara ili kujenga taifa lenye uwezo wa kujitengemea kiuchumi.
Katika shairi la “Tuzingatie Haya,” (uk .27 – 28) wasanii wanasisitiza umuhimu wa kufufua uchumi wa nchi. Pia ili tufufue uchumi wa nchi ni lazima tupunguze maneno na sote tufanye kazi kwa bidii, wananchi wote tuungane na kuhamasishwa (ubeti 2.) raia na viongozi sote tufanye kazi kwa bidii (ubeti 3) tuondoe tofauti zetu za tuepukane na tamaa ya utajiri. Beti za (2 na 4) zinasema:
2. Uchumi kufufua, si hotuba refu sana.
Moja litosaidia, ni kuhamasishana,
Jingine linalofuatia, sote kushirikiana,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.
4. Kufanya kazi lazima, tuacheni utegezi,
Na jingine la kukoma, kuwepo kwa uchaguzi,
Kutupiana lawama ni mambo ya kipuuzi,
Tuyazingatie haya, wala tusirudi nyuma.
Hapa inaonekana kuwa ili tuweze kuinua uchumi wa nchi ni lazima tuwahamasishe watu; tujenge umoja na ushirikiano, tuondoe ubaguzi na tufanye kazi kwa bidii.
Shairi hili, pamoja na mambo mengine linawataka viongozi waache kupora mali ya umma na badala yake washiriki barabara katika kujenga uchumi. Iwapo tutajenga uchumi imara tutaondokana na mtatizo yanayoonekana.Haya tunayapata katika shairi la Tunzo (uk.29 – 30).
Jambo la pili ambalo wasanii wanalisisitiza katika ukombozi wa kiuchumi ni umuhimu wa Kilimo.Wasanii wanasema kuwa iwapo tutazingatia Kilimo tutapata chakula cha kutosha na ziada ya kuuza nje ya nchi kwa ajili ya kujipatia pesa za kigeni na kwa ajili ya kuboresha maisha yetu. Iwapo utazingatia Kilimo tutaepukana na tabia au hali ya kutegemea chakula kutoka nje. Suala la kupata chakula cha kutosha litatuepusha na masharti magumu yanayoweza kupewa na watu wanaoweza kutupatia chakula pindi tunapopata tatizo la uhaba wa chakula.
Washairi wanadhihirisha haya kwa kutumia shairi la Adui (uk. 13)
4. Tulime jama tulime, tushinde adui njaa,
Hapa kwetu ituhame, kwingine kutokomea,
Wala sisi tusikome,, chakula kujilimia,
Tutie jembe mpini, tuteremke shambani
5. Chakula kujilimia, ziada kujipatatia,
Tuache kutegemea, vya nje kuagiza,
Siku watojigomea, nani tutamkimbilia
Tutie jembe mpini, tuteremke shambani
Katika shairi la “Mkulima” (uk. 3 – 4) linaonyesha mkulima kama mtu duni likimlinganisha na watu wengine. Huyu ni mtu ambaye analima ili kulisha watu wote nchini na kuinua pato la taifa, lakini hathaminiwi na watu wanaohusika.
5. Wakazi wa mjini, na wafanyakazi pia,
Na viongozi nchini, huduma awapatia.
Sijui kukosa nini, thamani kutomtia,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa
Hivyo basi, ili tuimarishe Kilimo ni lazima kumthamini mkulima. Na kumpa huduma muhimu anazostahili. Pia chakula kipunguapo nchini wa kutupiwa lawama ni mkulima ambaye hathaminiwi. Wanasema:
7. Upungufu wa chakula, utokeapo nchini,
Hukumbana na suala, shambani wafanya nini,
Kazi yako unalala, watia njaa nchini,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa.
Licha ya Mkulima kufanya juhudi kubwa katika kuinua uchumi wa nchi hapewi huduma muhimu, badala yake huduma hizo hupelekwa mjini; Kama wanasemavyo waandishi;
8. Starehe kwa jumla, zinaishia mjini,
Maji safi ya muala, njia na umeme ndani,
Aliyezichuma hela, ni Mkulima shambani,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa.
Hapa inaonyesha kuwa licha ya kwamba mkulima ndiye anayezalisha kila kitu.Wanaofaidi matunda ya Mkulima ni watu wa mjini. Ili tuweze kuinua na kuimarisha Kilimo chetu, ni lazima tumthamini mkulima na apewe misaada na huduma mbalimbali.
Kwa upande mwingine wasanii wanaonesha kuwa ili tuweze kujikomboa kiuchumi ni lazima tuachane na uzembe kazini. Washairi wanadai kuwa kuna baadhi ya watu hasa, wafanyakazi maofisini ni wazembe ,hawatimizi wajibu wao kama ipasavyo.pindi tu waingiapo ofisini wanajifanya wana kazi nyingi kiasi kwamba kiasi kwamba wanashindwa kuwahudumia wananchi kama wasemavyo washairi katika shairi la Puuzo (uk. 8).
-
Ofisini ukifika, wanajitia pirika,
Haja unayoitaka, mwenyewe tuhangaika,
Wajifanya hawajali
edu.uptymez.com
4. Baoni utapokaa, mwishowe tapakataa
Shida iliyokukaa, nayo yazidi chakaa,
Sababu puuzo zao
Wasanii hawa wanakemea tabia hiyo na kuwataka wanajamii wachape kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi. Uchapaji kazi huo lazima uanzie katika
ngazi ya chini kama vile familia, hadi kitaifa. Wafanyakazi, wakulima na wasomi wote sharti wachape kazi kulingana na majukumu yao ili kuteketeza adui
uzembe. Haya tunayapata katika shairi la Charuka (uk. 53 – 55).
Vilevile wasanii wanonesha kuwa ili tujikomboe kiuchumi tupige vita ukoloni mamboleo na unyonyaji. Ukoloni mamboleo ni hali ya nchi moja kuitawala
nchi nyingine kiuchumi. Hii inaathiri uchumi wa nchi maskini. Katika shairi la “22” Nipatieni Dawa,” jinsi ukoloni ulivyoondoka nchini inazungumzwa
lakini ukoloni huo umerudi kwa umbo lingine la ukoloni mamboleo. Kuja kwa ukoloni mamboleo, kuliendeleza taratibu na desturi za kunyonya uchumi wa
nchi masikini.
6. Pale pale penye donda, ndipo apojanibana.
Nikawa sasa nakonda, pumzi nikawa sina,
Nikabaki kama ng’onda, la kufanya sikuona,
Nipatieni dawa, nipate kutononoka.
7. Kila nikifurukuta, donda apate toa,
Najuta kwenye tata, shina kujizidishia
Dawa nimeshatafuta, ili nipate kutoa,
Nipatieni dawa, nipate kutononoka.
Beti hizi zinaweka wazi jinsi ukoloni mamboleo unavyozibana nchi maskini kiuchumi mpaka zinashindwa hata kupumua. Ili tujikomboe kiuchumi, ni lazima tufate dawa ya kuondoka ukoloni mamboleo hapa nchini. Kwa hiyo ili tujikomboe kiuchumi lazima tupege vita ukoloni mamboleo.
Ukombozi wa kiutamaduni
Katika ukombozi wa kiutamaduni wasanii wanazungumzia juu ya ukombozi wa mwanamke. Ukombozi wa mwanamke ni jambo la msingi na muhimu katika jamii. Mwanamke akikombolewa ni sawa na jamii nzima kukombolewa. Shairi la 10, “Kifungo”, waandishi wanasema;
7. Kwa kuwa ni mwanamke, ndani mnanifutika
Lazima nje nitoke, kupata ninayotaka,
Nimechoshwa na upweke, sitaka kudhalilika,
Kifungo kimenichosha, minyororo nafungwa.
Ili aweze kujitegemea mwenyewe, mwanamke anahitaji kuwa huru, na siyo kufugwa fugwa ndani na kumtegemea mwanamme.
“Hina inapapatuka” Linaonyesha jinsi mwanamke alivyogandamizwa na mwanaume hapo zamani:
-
Zamani tukikumbuka,watiaji walivia,
Nyumbani katu kutoka, ndani walijichimbia,
Mabwana walitamka, marufuku kutembea,
Unyonge inaondoa, Hina inapatikana.
edu.uptymez.com
Hapa wanaonyesha kuwa mwanamke hakuruhusiwa kwenda kutembea. Mwanamke aliwekwa utawani na kazi yake kubwa ilikuwa kupika chakula.
Hakuruhusiwa kabisa kusoma na kuandika.
Hata hivyo mabadiliko ya jamii kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni yanamkomboa mwanamke kidogo kidogo. Kwa wakati huu nao wanafanya kazi mbalimbali ambazo hapo zamani hawakuruhusiwa kuzifanya kwa mfano:
7. Leo wanamakanika, hadhi yao kutetea,
Kila mahali kufika, na wao wameenea,
Kazini wajumuika, shime wanajifanyia.
Unyonge inaondoa, hina inapapatuka.
8. Kila utapopashika, nao wameshafika,
Zege inapopondeka, ni wao hujipondea,
Matofali kupeleka, mafundi kusaidia,
Unyonge inaondoa, hina inapapatuka.
Kujikomboa kwa mwanamke kunatokana na juhudi zake chini ya Umoja wa Wanawake ambao umewaongoza wanawake katika kudai haki zoa na kuondoa dhuluma wanazofanyiwa na wanaume (ubeti 6).
Kwa sasa, wanawake wanajua kusoma na kuandika (ubeti 9) wengine wamejiunga na jeshi (ubeti 11) na wengine ni viongozi (ubeti wa 10).
Tena wananasisitiza kuwa, wanawake washikilie uzi walio nao. Wasipunguze mkazo bali wakazane ili waufikie ukombozi wa kweli, utakaowapa uhuru wa kuamua mambo yao wenyewe bila kuingiliwa na wanaume (ubeti 14).
Ukombozi wa Kisiasa
Katika shairi la “Samaki Mtungoni,” (uk. 19) linaonyesha harakati za watu wa tabaka la chini kuondokana na utumwa wa kutawaliwa na kugandamizwa na mkoloni. Samaki anaashiria watu wa tabaka la chini wanaonyonwa na kugandamizwa; Na mvuvi ni wakoloni au tabaka tawala.
Ukombozi wa Kifikra
Katika shairi la “Usiwe Bendera” (uk. 31) linazungumzia juu ya ukombozi wa kifikra na kimawazo.jamii inatahadhariswa isiwe bendera kufuata kila uelekeo wa upepo bali ijitegemee kimawazo.
Dhamira nyinginezo.
- Matabaka
edu.uptymez.com
“Samaki Mtungozi” linaonyesha matabaka ya aina mbili: tabaka la chini (samaki) na tabaka tawala (mvuvi). Tabaka tawala linanyonya na kulingandamiza tabaka tawaliwa.
Shairi la 14, “Punda” waandishi wanaonyesha jinsi tabaka la chini linavyotumikishwa kwa kulinganishwa na punda.
“Nini Wanagu” inaonyesha hali ya maisha ilivyongumu na duni kwa tabaka hili la chini ambalo halina kitu, ukilinganisha na tabaka la juu.
Shairi 2,”mkulima” linaonyesha jinsi mkulima asivyothaminiwa na tabaka la juu (viongozi).Mpaka inafikia hatua ya kumyima hata huduma muhimu anazo ta kiwa kuzipata.
- Uongozi mbaya
edu.uptymez.com
Katika kujadili dhamira hii waandishi wameonyesha kuwa uongozi uliopo hauwajibiki na hivyo ni mbaya.
Shairi la 5 “Puuzo” linazungumzia jinsi viongozi wasivyotoa huduma zinazotakiwa maofisini mwao, badala yake husumbua watu wanaohitaji huduma hizo:
2. Unapokuwa na shida, wao wanakupuuza
Watajitia kidada, na kuifanya ajiza,
Wajifanya hawajali.
3. Ofisini ukifika, wanakuweka baoni
Wakati uliofika, wao hawathamini,
Wanakwambia subiri.
Shairi la 4, “Bahari‘ inazungumzia jinsi viongozi wanavyowadhulumu raia haki zao:
7. Hudai ni haki yao, Mola amewajalia.
Kuwadhulumu wenzao, wao wanafurahia,
Nao kwa unyonge wao, wadogo wateketea,
Bahari ina hatari, wala usiichezee.
“Mpaka Lini” inahusu jinsi viongozi wamejitia uziwi ili wasisikilize matatizo ya raia na wasivyotatua matatizo yao. Viongozi huwakumbatia wasema uongo na wasema kweli hunyanyasika.
Katika shairi la 32. “Payuka” wasanii wanaonyesha jinsi viongozi wetu wanavyopayuka ovyo na kuahidi mambo mengi wakiwa jukwaani lakini hawatekelezi yale wanayoongelea. Badala yake,wanabaki kuwaonya na kuwanyanyasa wananchi.
- Umuhimu wa kutatua matatizo katika jamii
edu.uptymez.com
Matatizo ya jamii ni mengi mno hasa baada ya kupata uhuru wa bendera. Hivyo ni vyema yashughulikiwe ili kuepusha migongano na majungu ambayo yanaweza kujitokeza na kuchukua sehemu kubwa ya muda wa kujenga nchi yetu.
Shiri la 19. “Tunzo,” wasanii wanazungumzia umuhimu wa kutatua matatizo mbalimbali katika jamii yetu ili tuweze kuishi kwa Amani. Matatizo ni kama vile, ongezeko la watu (ubeti 2), kuanguka kwa uchumi (ubeti 3) maradhi mbalimbali (ubeti 3), ubaguzi (ubeti 4) n.k. matatizo hayo yanatatuliwa kwa ushirikaino wa watu wote katika jamii:
6. Kwenu ninalo tamko, kwa yote jamii nzima fuatizo,
Sote tuwe unganiko, kina baba kina mama ni himizo
Tuondoshe sawijiko, ili yapate tuhuma matatizo.
7. Tuyatende kwa pangiko, ili yasije tukwama mzozo,.
Tufanye kimzunguko, vijana watu wazima saidizo,
Tulipata ongezeko, la mazao yenye nema na uwezo.
- Mapenzi na ndoa
edu.uptymez.com
Katika kuongelea suala la mapenzi wasanii wamejaribu kugusia hata mapenzi ya watu wawili ambao tayari wako katika ndoa. Katika kujadili suala hili la mapenzi msanii anaanza kumsifia mwanamke ampendaye. Wanasema kuwa mwanamke huyo ni mzuri sana kiasi kwamba kila mtu huvutiwa na uzuri wake. Haya yanadhihirishwa na shairi la Ua (uk. 21 – 22) lisemalo,
3. Rangi yake ya sanaa, machoni inavutia
Ukiliona lang’aa, moyoni lakuingia,
Ua sasa limejaa, macho walikodolea.
Wasanii wanadai kuwa ataendelea kumpatia matunzo ili wengine wasimpatie na hatimaye awe mwenzi wake siku itakapofika. Wasanii wanasema,
7. Nami sitoliachia, matunzo talipatia,
Hadi nitapofikia, mkononi kulitia,
Ua sasa limepea, macho walikodolea
Kutokana na mapenzi ya dhati aliyonayo mshairi huyo, anatoa majonzi yake kwa mwenza wake aliyeishi naye kwa muda wa miaka sita kabla ya kifo kumchukua. Anadai kuwa mpendwa wake huyo alikuwa na tabia nzuri na hakuwa na matatizo yoyote. Haya yote yanadhihirishwa na shairi la Nipate Wapi Mwingine (UK. 32 – 33),
- Njiwa ali maridadi, kwa tabia hana shaka,
edu.uptymez.com
Na hakuwa mkaidi, umwitapo kakufika,
Mfanowe kama radi, chini inapoanguka,
Njiwa ameshanitoka, nipate wapi mwingine?
Hata hivyo, washairi hawa anakemea mapenzi yasiyo ya kweli, yaani wanalaani mapenzi yasio ya dhati. Wanasema kuwa kuna baadhi ya wanaume hawana mapenzi ya dhati kwa wake zao. Watu hawa huwaacha wake zao na kuvinjari na vimada. Shairi la kwa nini? (Uk. 1 – 2) linadhihirisha haya
4. Mke wake, atamwacha,singizini,
Atoroke, parakacha, migombani,
Kumbe kake, anakochani, mwa jirani,
Kwa nini?
Wasanii wanaendelea kulaumu mapenzi ya ulaghai katika mashairi ya kuunge (uk. 25) utanikumbuka (uk. 44) na Kitendawili (uk. 14). katika shairi la kuunge wasanii wanasema kuwa katu hawakubali kushiriki na mtu asiye na msimamo katika mapenzi. Anasema:
2. Silipandi asilani, gogo lilokauka,
Naraduwa kuwa chini, japo nitahangaika,
Mnaosema semeni, kisha mutapumzika.
Wasanii wanasema kuwa hawataki mtu kama huyu ili kuepuka maafa ya kimapenzi ambayo yamewahi kuwapata wengine.
Vilevile, katika shairi la Kitendawili, wasanii wanaendelea kulaumu tabia ya baadhi ya watu ambao hawatuliii katika mapenzi yaani wanafanana na jongoo ambaye hawezi kutulia kwa mfugaji wake.
Pia, katika shairi la “Utanikumbuka” mshairi anamwambia mpenzi wake ambaye amemsaliti kuwa atamkumbuka siku za badayae kutokana na ukweli kuwa msanii alishamtendea mambo mengi sana ambaye aliyemlaghai hataweza kumtendea. Anasema.
3.Umeona bora kitu,ukasahau ya nyuma,
Umetupa mbali utu, na zote zangu huruma,
Kwako kutokaa katu, ipo siku utakwama,
Utaumiza uwatu, iwe na yako hatima.
Kupiga vita unyonyaji
Wasanii wa diwani hii wanaosha kuwa katika jamii yetu kuna unyonyaji wa hali ya juu kama ilivyokuwa enzi za ukoloni. Katika shairi la Bahari (uk 6 – 7) linaonesha waziwazi jinsi viongozi wanavyowanyonya watawaliwa. Shairi hili linasema.
6. Suala wajiuliza, katika jamii zao,
Wanaona miiujiza, wanayotenda wenzao,
Wakubwa wanajiweza, kula wadogo zao,
Bahari ina hatari wala usichezee.
Shairi hili linaendelea kudai kuwa kitendo cha viongozi kuwanyonya wazalishaji mali mumehalalishwa na viongozi wenyewe. Viongozi wanaona kuwa kunyonya wananchi wakawaida ni haki ya msingi waliyopewa na mwenyezi Mungu. Kitendo ambacho washairi wanakataa. Washairi wanaonesha unyonyaji wa aina hii katika shairi la “Samaki Mtungoni” (Uk. 19 – 20) .katika shairi hili tunaona samaki (watawaliwa) wakinyanyaswa, kuuliwa na kunyonywa na mvuvi (mkoloni au mtawala).Hali hii imesababisha kutoweka kwa utu wa samaki (watawaliwa) kama asemavyo mshairi.
5. Haki yao mepotea, na heshima kuondoka,
Mebaki waninginia, mtungoni mepangika,
Bwana amechachama, nyumba kwenda kupika,
Leo wako mtongoni, huzuni inawakumba.
Washairi wanadai kuwa, pamoja na kuondoa ukoloni nchini, bado hali za wa nanchi wa kawaida ni mbaya sana. Haya yote tunayopata katika shairi la “Hali Halsi” uk. 5) ambalo linaonesha hali tete kwa mwananchi wa kawaid
4. Nuru tuliieneza, giza kulitokomeza,
Wote wasiojiweza, hali kuzifananiza,
Mshumaa unawaka, giza mbona limezidi?
Kwa vile hali za wananchi zinazidi kuwa mbaya tangu enzi za mkoloni hadi leo, washairi wanawataka wanajamii wafanye mapinduzi ya kweli dhidi ya unyonyaji na ukoloni wa aina yoyote. Haya yote yanapatikana katika mshairi ya Sokomoko
baharini (uk. 63 – 64) Haki (uk 47 – 48) na Payuka (uk 50 – 52). Mashairi haya yote yanatoa mwamko wa kisiasa, mwamko wa kuleta mabadiliko katika jamii ili haki ipatikana”.Katika shairi la Sokomoko Baharini, mshairi anakusanya vijana na wanyonywaji ili waungane kwa pamoja na kwa lengo la kuleta mabadiliko. Anasema,
10. Hapa mbele sirudi tena, nia mimi nimechukiwa,
Nenda kusanya vijana, hali wanaoijuwa,
Matumbo yalokunjana, wa tayari kuambiwa,
Mashua kuiokoa, mbio watakimbia.
Shairi la Haki linaendelea kuamsha mioyo ya wanyonge ili wapambane dhidi ya unyonyaji na ukoloni, Shairi hili linawataka wanajamii watafute haki yao ambayo imetekwa na watawala wao. Shairi linasema
8. Haki husimama, kwa Viumbe sisi, tuvyojaaliwa,
Na huna ulimi, kuweza tukasi, tukageukiwa,
Zama za uchumi, zishashika kasi, nguvu zishapewa,
Haki wauliwa
Mashairi hayo yanafanana na utenzi wa Payuka unaowataka wanajamii wamke na kupigania haki zao ambazo zimevizwa na baadhi ya watu kama vile watawala wao au wakoloni. Utenzi huu unasema,
16. Amkeni amkeni,
Msilale asilani,
Vibaya mnaumia
6.Maadili mema na maonyo katika maisha.
Katika diwani hii, wasanii wamejaribu kuwaadili na kuwaonya wanajamii ili waweze kuishi maisha bora. Katika
kuzungumzia suala hili, wasanii amegusia masuala yafuatayo:
Moja, matumizi mazuri ya fedha. Wasanii wanaitaka jamii kutumia vizuri pesa inazozipata. Wasanii wanasema kuwa iwapo jamii itatumia pesa zake vibaya itakuja kujuta siku za baadaye. Wanajamii wanatakiwa kutunza pesa vizuri ili kujenga maisha yao ya baadaye. Haya tunayapata katika utenzi wa Israfu (u. 17 – 18).
6. Huu ni wakati wako,
Kujenga kesho yako,
Kuepuka chokochoko,
Za hao adui zako,
Mwenzangu nakuisia, Israfu haifai.
Hivyo, tutumie vizuri fedha zetu ili kuepukana na majonzi au majuto tunayoweza kuyapata siku za baadaye.
Mbili, umuhimu wa kusema ukweli, Wasanii wanawataka wanajamii kusema ukweli daima. Katika shairi la Ulimi (uk. 41) wasanii wanaziasa ndimi zao tusiropoke bali ziseme ukweli tupu. Hali hii itasaidia kulinda heshima yao katika jamii. Shairi hili linasema.
3. Usiropokeropoke, kwa wenzio kwanza sema,
Usipachikepachike, maneno yasiyo mema,
Useme wanufaike, kwa kauli yako njema.
Ewe ulimi sikia!
Wasanii wanaendelea kudai kuwa kwa vile ulimwengu umejaa shida, lakini shida hizo zisiwe chanzo cha kusema uongo.Hayo tunayapata katika shairi la Ulimwengu (uk. 42 – 43) ubeti wa 3.
Shida dhiki ni halali, haramu ikijibari,
Ni bora kutoa kweli, uongo uso wa nari,
Ni vyema kutakabali dhila na zake hatari,
Ulimwengu!
Ukweli husaidia kujenga jamii iliyo bora, husaidia kuondoa wale wote wenye nia ya kubaguana, hasa katika masuala ya dini, rangi na hata kabila. Haya yote tunayapata katika shairi la Pasua Uwape Ukweli. (uk 46).
Nalo shairi la “Mwabwaja Mwasema Nini“? (uk. 61 – 62) linadhihirisha dhana ya kusema ukweli kwa kuwataka watu waseme ukweli kwa vitendo. Washairi wanawataka waandishi waseme ukweli kuhusu hali halisi ya maisha ya watu wa kawaida. Vilevile, anawataka waandishi watekeleze kwa vitendo wanayoyasema. Kusema ukweli na kutenda mambo yasemwayo itasaidia sana katika kujenga jamii iliyo bora.
Tatu, umuhimu wa kutenda mema. Wasanii, wanawausia wana jamii kutenda mema kwani mtu yeyote atendewaye mema anastahili kulipa kwa wema aliotendewa, hata kwa kusema ahsante. Na yeyote atendaye mema atalipwa kwa njia yoyote ile, ikiwemo ya kiroho. Katika shairi la “Hisani Hulipwa” (uk. 45) tunaambiwa kuwa,
3. Akufichiae,siri, zinonuka,
Na akurambae, akakusafisha,
Akutafutae, unapopotea,
Hisani hulipwa.
Nne ,ni kuachana na anasa za dunia.Wasanii wanawaasa wanajamii kuachana na tamaa za kimaisha. Shairi la Siharakie Maisha (uk 11 – 12) linawaasa wanafunzi kuachana na papara za kimaisha na badala yake wasome kwani maisha ni kama kupanda mnazi ambapo mpandaji sharti aanzie shinani kama atakiwavyo mwanafunzi kutong’ang’ania mambo ya anasa za dunia kama vile umalaya, ulevi, uchoyo, wizi n.k. bali ajijengee ya kesho, yaani asome kwa bidii ili apate elimu bora ambayo ndio msingi wake wa maisha ya baadaye. Shairi hili linasema,
2. Ubado ni mwanafunzi,
Usingiwe na simanzi,
Ruka vikwazo ja panzi,
Ipambe yako enzi,
Maisha safari ndefu, kutembea usichoke.
3. Somo babo endelea,
Sicheze pata potea,
Muda wako ukimea,
Maisha kufurahia,
Usiache kutegua, kwa kutegemea tega
Wasanii wanaendelea kudai kuwa raha za dunia hazina thamani kwani waliowahi kupata raha sasa wanajuta. Wanaonesha kuwa watu hao pindi wapatapo pesa huwasahau wengine kwa kuwaona kama hawafai huyafakamia maisha kabla dunia haijawafundisha. Haya yote tunayapata katika shairi la Raha (uk – 24) ambapo mponda raha anajuta,
4. Leo raha naiwacha, atakaye aje kwetu,
Nami nataka kututa, nitulie kama watu,
Nimechoka kuzorota, nakubakia sukutu,
Chukueni mtumie.
7.Umuhimu wa kutumia pesa vizuri.
Matumizi mabaya ya fedha ni kujitia kwenye umasikini, na mali bila daftari hupotea bila kujua. Katia diwani hii, waandishi wanaonyesha au wanasisitiza juu ya matumizi mazuri ya pesa.
Katika shairi la 11, “Israfu” wasanii wanaionya jamii juu ya matumizi mabaya ya fedha zinazopatikana:
1. Mali ulijichumia,
Ni yako nakubalia,
Lakini kuangalia,
Vipi unaitumia,
Mwenzangu nakuusia Israfu haifai.
Wasanii wanaonyesha kuwa matumizi mabaya ya fedha husababisha umasikini kwa muhusika na umaskini husababisha akimbiwe na watu wote hata marafiki zake.
8. Athari ya sukari mwilini
Sukari ni kitu cha muhimu sana katika mwili wa binadamu. Lakini sukari hiyohiyo ikizidi inaleta madhara mbalimbali mwilini.
Katika shairi la 34 “Sukari” Wasanii wanaonyesha madhara mbalimbali yatokanayo na sukari kuzidi katika mwili wa mwanadamu. Athari hizo ni kama vile meno kung’oka (ubeti 2)
Pia sukari huleta safura mwilini na ugonjwa wa kisukari.
Ujumbe (Maadili mabalimbali)
1. Kuinua uchumi wa nchi ni jambo la muhimu sana, ili tuweze kuondokana na utegemezi wa kutegemea misaada toka nje.
2. Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu, hivyo ni lazima tukiimarishe na Mkulima lazima athaminiwe.
3.Ukombozi wa mwanamke ni muhimu sana, kwani mwanamke akikombolewa atazijua na kudai haki zake kwa ujasiri,na atakuwa msaada mkubwa zaidi kwa jamii.
4. Ni muhimu kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yetu ili tuweze kuishi kwa Amani na utulivu.
5. Ni vizuri kuwa na maadili yaletayo kutendeana mema katika jamii, kwani kufanya hivyo tutajenga jamii yenye haki na usawa.
6. Ni vizuri kuwa na matumizi mazuri ya pesa zetu ili kuukwepa umasikini.
Falsafa (Mwelekeo)ya Waandishi
Waandishi wanaamini kuwa tukisisitiza Kilimo na kumthamini mkulima tutainua uchumi wetu kwa kiasi kikubwa. Pia wanaitaka jamii ifuate misingi ya haki na usawa katika maisha. Wanatetea haki na usawa kwa watu wote.
Msimamo wa Wandishi
Waandishi wana msimamo wa kimapinduzi kwani wamejadili masuala mbalimbali ambayo ni nyeti kwa jamii yetu na kukemea uonevu kwa ujumla.
Fani
Muundo
Miundo changamano umetumika. Kuna muundo wa tathlitha (mistari mitatu)- shairi la 5 “Puuzo” 13 “Ua,” na 32 “Payuka“: tarbia (mistari minne) – shairi la 4 “Bahari“/ 2 “Mkulima” 20 “Usiwe Bendera” 27 “Utanikumbuka” na sabilia au takhmisa (mistri mitano na kuendela) shairi la 7 “Siharakishe Maisha”/“11 Israfu” na 14 “Punda“.
- Mtindo
edu.uptymez.com
Waandishi wametumia mtindo unaofuata kanuni za ushairi wa kimapokea na urari wa vina na mizani kwa mshairi mengi, mfano shairi la 2,3,4,6,8,9,10,12, n.k. Pia wametumia mtindo unaofuata ushairi wa kisiasa kwa mfano katika shairi la 19.
Matumizi ya Lugha.
Lugha waliyoitumia waandishi ni ya kishairi yenye methali, tamadhali za semi, mbinu nyingine za kisanaa na taswira mbalimbali.
Methali
- Subira yavuta heri (shairi la 7 ubeti 8)
- Aisifuye mvua kaloa mwilini mwake (shairi la 23 ubeti 12)
- Fahari wapiganapo nyasi ndizo huonewa (shairi la 37 ubeti 7)
- Misemo:
- Siharakie maisha (shairi la 7).
- Kusumbukia kichaa (shairi la 23).
- Sokomoko baharini (shairi la 37).
edu.uptymez.com
- Tamathali za semi
- Tushibiha
edu.uptymez.com
Ubaguzi umezama kama nguzo (shairi la 19 ubeti 4).
Maisha ni kama njia (shairi la 24).
- Tashihisi.
edu.uptymez.com
-Katika shairi la “Samaki Mtungoni” Samaki wamepewa uwezo wa kibinadamu.
-Katika shairi la “Nipate Wapi Mwingine“. Hapa njiwa amepewa uhai kama mpenzi aliyefariki.
- Mbinu Nyingine za Kisanaa.
- Tashtiti – katika shairi la “Mwabaja Mwasema Nini?” mfano– Nasikia mnatunga, mwatungani washairi?
- Tanakali sauti – mfano katika shairi la “Kwa Nini“! – neno parakacha, shairi la “Mkulima” neno kokoriko n.k.
- Takriri – kuna matumizi kurudiarudia maneno katika mashairi ya “Kifungo” – “Adui” “Majonzi” n.k
edu.uptymez.com
Ujenzi wa Taswira
Njiwa – Mpenzi -katika shairi la “Nipate Wapi Mwingine?’
Samaki – Watu wa tabaka la chini
Mvuvi – Watu wa tabaka tawala – shairi la “Samaki Mtungoni”
Punda – Tabaka la chini linalonyonywa na kuagandamizwa
Ua – Mwanamke au msichana.
- Jina la Kitabu
edu.uptymez.com
Jina la diwani hii , Malenga Wapya linaendana na makusudio ya watunzi. Neno malenga lina maana ya mshairi na neno wapya lina maana ya watu au vitu ambao au ambavyo ni wa / vya kisasa. Hivyo Malenga Wapya lina maana ya washairi wapya. Hali hii inatufanya tuamini kuwa jina Malenga Wapya linaendana na hali halisi ya mambo yaliyo ndani ya diwani hii kwa kuzingatia nyanja kuu, mbili:
Kwanza katika utangulizi tunaambiwa kuwa Malenga Wapya ni mkusanyiko wa mashairi 37 yaliyotungwa na wanafunzi mbalimbai katika kipingi cha uwanafunzi wao (uk. 5) kwa maneno mengine Malenga Wapya lina maana ya washairi wapya au washairi vijana (wachanga) walioamua kuingia katika uwanja wa ushairi.
Pili, malenga wapya lina maana ya washairi wapya wanaotumia mitindo mipya ambayo imo ndani ya diwani hii. Kusema ukweli diwani hii ina upya fulani, hasa kwa upande wa mtindo. Upya huu ni nadra kuupata katika diwani nyingine, ingawa mtindo uliotumika wa kimapokeo peke yake. Hata hivyo mtindo huu umeibua mshairi yenye mitindo tofautitofauti. Jambo hili linaifanya diwani hii ionekane mpya au ionekane tofauti na diwani tulizowahi kusoma. Upya huu kimtindo, unaweza kuelezwa kama ifuatavyo:
Diwani hii ina baadhi ya mashairi yenye vina viwili vya kati tofauti na diwani zilizo nyingi, ambazo tumewahi kusoma. Kwa mfano, katika shairi la “Tunzo” (uk. 20) tunaona hali hii,
8. Tulete mabadiliko, huku nia iwe njema, tangu mwenzo,
Matumaini yaweko, tukijachagua mema, kimawazo,
Tena aliadi, iweko, kwa nchi yetu nzima, endelezo.
Tukichunguza shairi hili tutaona kuwa kuna vina vya kati vya aina mbili, ambavyo ni “ko” na “ma” kama vinavyoonekana ndani ya shairi. Shairi jingine lenye vina vinavyofanana na hilo ni “Haki” (uk 47 – 48).
Vilevile, kuna upya mwingine katika utumiaji wa mizani. Baadhi ya mashairi kama vile “Usiwe Bendera (uk 31) na Hisani Hulipwa” (uk. 45) yana mizani 12 badala ya 16 au 8 kama ilivyozoeleka katika mashairi ya kawaida na tenzi zenye kufuata kanuni za kimapokeao. Shairi la Usiwe Bendera linathibisha haya,
1.Kaa ufikiri, ni tokueleza,
Haya udhukiri, ukiyachunguza,
Hujawa mazuri, hwenda yakatunza.
Ubeti huu una mizani 12, kwa maana kuwa kila nusu mstari una mizani 6 Mwisho, washairi hawa wametumia mtindo wa tenzi ambao pia una upya fulani. Upya huo unaonekana katika mstari wa mwisho ambao una mizani nyingi tofauti na mistari mingine ya tenzi ambayo kwa kawaida huwa na mizani 8. Lakini mstari wa mwisho una mizani 16. Hali hii inajionesha katika tenzi za Siharakishe Maisha. (Uk 11 – 2) Israfu (uk. 17 – 8). Mfano mmojawapo ni ubeti wa 2 wa utenzi wa Sibarikie Maisha.
Ubado ni mwanafunzi
Usingiwe na simanzi
Ruka vikwazo ja panzi
Uipambe yako enzi,
Maisha safari ndefu, kutembea usichoke.
Tunaweza kusema kuwa ingawa hakuna upya wowote kimaudhui lakini kifani kuna upya mwingi. Upya huu, ikiwa ni pamoja na uchanga wa watunzi au washairi ndio unaotufanya tusema kuwa jina la diwani Malenga Wapya linasadifu yale yaliyomo ndani yake
- Kufaulu kwa Mwandishi.
edu.uptymez.com
Kimaudhui
-Mwandishi amefanikiwa kutuonyesha dhamira mbalimbali ambazo zinaonyesha maisha yetu kabla ya uhuru na baada ya uhuru mpaka sasa.
-Waandishi wameonyesha mvutano kati ya tabaka la chini na tabaka la juu (uongozi mbaya, n.k)
-Wameshauri jamii kuwa na maadili mema.
-Waandishi wameonyesha matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi yetu.
Kifani
-Wamefanikiwa kutumia lugha ya kishairi, nyepesi na yenye taswira.
– Kimuundo mashairi yao yanajitosheleza.
Kutofauulu kwa Waandishi
Kimaudhui
-Waandishi katika mashairi ya “Mkulima” na “Adui” wameonyesha ukasuku walionao kwani tangu zamani za kale hadi leo hii watu wamekuwa wakilima lakini bado hali zao ni duni.
-Wamerudiarudia maneno yanayoimbwa majukwaani kuhusu viongozi badala ya kutuonyesha njia za kisayansi nakiteknolojia za kuondokana na matatizo ya kiuchumi, kifikra na kijamii.,
-Aidha wasanii wamekuwa na mtazamo potofu na dhaifu katika kutoa baadhi ya maadili mfano: shairi la “Hisani Hulipwa”
Kifani
Diwani hii imetumia lugha rahisi kiasi kwamba hamfikirikishi msomaji.