TAMTHILIYA
Jina la Kitabu: ORODHA
Mwandishi: STEVE REYNOLDS
Wachapishaji: MACMILLAN
Mwaka: 2006
(a) PITIO LA KITABU
Orodha ni tamthiliya ambayo inaonyesho moja na onyesho lenyewe lina sehemu ishirini (20).
Sehemu ya kwanza
lnaanza kwa kuonyesha vifani vinne vimeganda. Kifani cha kwanza, wahusika wameganda katika mikao inayotambulisha wasifu wa wahusika. Kifani cha pili kinaonesha wagonjwa wakiwa katika mateso. Kifani cha tatu kinaonesha wahusika wakiwa katika maumivu makali sana.
Sehemu ya pili
Ni siku ya msiba wa Furaha. Padri James yupo Kwa ajili ya mazishi. Mama yake Furaha anaeleza umati wa watu kuwa Furaha aliacha barua yenye orodha. Mama Furaha anaomba asome hiyo barua.
Anasema, ningependa kusema maneno machache kuhusu Furaha, binti yangu aliyetutoka.”Padri James anajaribu kumzuia mama Furaha asiseme yale aliyoombwa na Furaha enzi za ugonjwa wake.
Padri James anasema, ‘Mama Furaha, ninapinga! Haya ni majishi na wala si onyesho la pembeni la futuhi! Hapa si mahali pa…” (uk. 3)
Habari za uwepo wa barua yenye orodha inaleta hofu kwa watu wengi kijijini. Kwa mfano, Bw.Ecko anakiri hili kwa kusema,
“Lazima nikiri nina wasiwasi kuhusu maudhui ya hiyo barua…”
Sehemu ya tatu
Sehemu hii inatuonyesha maisha ya familia ya Furaha. Baba yake Furaha akiwa anasubiri chakula anatoa maelekezo kwa Furaha kuwaelekeza wadogo zake ili wafahamu tabia njema. Baba hafurahishwi na mwenendo wa mwanae Furaha na kumtamkia maneno mabaya. Anamuonya kuwa kwa mwenendo alionao hatapata mtu wa kumuoa isipokuwa “Washamba wa kule baa.”
Sehemu ya nne
Chumbani kwa furaha na ndugu zake wamelala kwenye kitanda kimoja. Wamejifunika shuka moja. Mary anasikika akimwamsha Furaha watoroke. Dada mdogo wa Furaha anaamka na kumshitukiza dada yake (Furaha) kuwa anataka kutoroka kwenda kwa wanaume. Anatishiwa na Furaha kuwa akimwambia mtu atamchinja.
Sehemu ya tano
Mary na Furaha wanaingia baa, wanawakuta jamaa zao Ecko na Juma. Wanakunywa na kucheza. Anaona pombe ile ni chungu kwake. Mary anamshauri Furaha anywe na awe mwema kwa Ecko. Maana atamnunulia vitu vingi.
Sehemu ya sita
Furaha amekwenda kuungama dhambi zake kwa padri James. Alikunywa pombe na kukutana na wanaume hivyo alikuwa na dhambi za kutubu. Padri James anamshauri Furaha aje kesho yake saa moja usiku katika chumba chake cha kujisomea, nyuma ya nyumba ya kanisa. Padri anamueleza Furaha kuwa mlango utakuwa wazi na taa zitakuwa zimezimwa kuficha utambulisho.
Furaha alifika kama alivyoagizwa. Padri anashikwa na tamaa za mwili na kuarnua kumliwaza Furaha. Ni ungamo ambalo analikiri.
Sehemu ya saba
Baba Furaha anakabiliana na Furaha sebuleni. Anamuonya Furaha kuhusu ulevi na umalaya. Furaha anaomba msamaha kwa baba yake. Mama Furaha naye anamuonya Furaha na kumtahadharisha.
Sehemu ya nane
Kitunda anasikiliza muziki. Furaha naye anaungana naye. Alikuwa ametumwa sokoni na mama yake. Wanazungumzia maisha ya Dar-es-Salaam. Furaha anababaika sana anaposikia kuhusu uzuri wa maisha ya Dar-es-Salaam. Kitunda anajaribu kumshawishi Furaha kuvuta bangi. Hata hivyo Furaha hakubali.
Sehemu ya tisa
Salimu anaingia kijijini kutoka Dar-es-Salaam. Alikuwa huko kwa muda wa miaka miwili. Wanakutana na Mary, habari zinamfikia Furaha. Salimu na Furaha ni wapenzi wa siku nyingi. Furaha akiwa na wasiwasi wa kuachwa na mchumba wake wa zamani (Salimu), Salimu anaingia nyumbani kwa Furaha.
Sehemu ya kumi
Salimu na Furaha wanakutana na kusalimiana. Wanaulizana mambo yaliyopita na kuelezea hatima ya mahusiano yao.
Sehemu ya kumi na moja
Wanakijiji wanazungumzia ujio wa Salimu. Wanazungumzia pia mahusiano ya Salimu na Furaha. Wanakijiji wanasikitishwa na tabia ya umalaya wa Furaha. Wanaionea huruma familia ya Furaha. Wankijiji wanamtaarifu mama Furaha kuhusu mwenendo wa mwanae.
Sehemu ya kumi na mbili
Mama Furaha anaamua kumuuliza Furaha ili kupata ukweli. Furaha anakataa kukiri tuhuma. Hata hivyo, hali yake inaonekana kudhoofu kwa kuumwa kikohozi na magonjwa mengine. Mama yake anahofu hali ya mwanae. Kwake hicho hakikua kikohozi tu, homa, malengelenge mwili mzima, mitoki, kupungua uzito kwa kasi, kukohoa damu, malaria vilimpa wasiwasi kuhusu afya ya mwanae.
Sehemu ya kumi na tatu
Furaha yupo sebuleni kapiga magoti akisali. Baba yake Furaha anamhoji mwanae Furaha kuhusu afya yake. Anamweleza binti yake kuwa ahakikishe ameolewa na Salimu.
Sehemu ya kumi na nne
Hali ya Furaha inazidi kuwa mbaya. Mama yake anaamua kumpeleka kwa daktari kuchukua vipimo vya damu. Furaha anagundulika ana UKIMWI. Mama Furaha pia anamuuliza Furaha kama amewahi kulala (kuternbea) na Salimu. Mama furaha anamweleza bintiye njia kuu zinazotumika kueneza UKIMWI.
Sehemu ya kumi na tano
Wanakijiji wanaeneza habari za ugonjwa wa Furaha wanajadili namna mtu anaweza kuupata ugonjwa huo. Habari za kuwepo kwa orodha iliyoandaliwa na Furaha zinazagaa na kuleta hofu kijijini hapo. Bw.Ecko, Salimu, padri James, Juma na Kitunda wana wasiwasi na mambo mawili:
(i) Kuambukizwa UKIMWI
(ii) Majina yao kuwa katika orodha hiyo.
Sehemu ya kumi na sita
Salimu anamtembelea Furaha baada ya kutoonana muda mrefu. Furaha anamweleza Salimu kuwa amekuwa mgonjwa muda mrefu kiasi hawezi kusimama. Salimu anamueleza Furaha kuhusu maneno anayosikia mtaani hususani hiyo barua yenye orodha. Furaha anaamua kumueleza Salimu kuwa ana UKIMWI. Salimu anachanganyikiwa na kudhani kuwa kaambukizwa. Hata hivyo anajipa moyo kwa kuwa wakati wote wamekuwa wakitumia kondom. Salimu anahitaji kuiona hiyo barua na mama Furaha anaingilia kati kuwa hapaswi kumtendea hivyo Furaha. Mama Furaha anamtia moyo Furaha na Furaha analala usingizi wa milele (amekufa).
Sehemu ya kumi na nane
Padri James anaomba radhi kwa lugha yake ya maudhi. Anawapa pole kwa msiba. Mama Furaha anamweleza padri James kuwa Furaha aliacha barua ambayo ingepaswa kusomwa siku ya mazishi. Padri James anaomba kuiona kwanza kabla hajairuhusu isomwe. Mama Furaha anakataa kumpatia. Anaachwa sebuleni peke yake. Padri James anatumia nafasi hiyo kuitafuta barua bila mafanikio.
Sehemu ya kumi na tisa
Ni asubuhi ya siku ya mazishi. Ecko, Juma na Salimu wanaonekana wakitafakari namna ya kuhakikisha barua haisomwi wakati wa mazishi ya Furaha. Hata hivyo wanashindwa kupata namna sahihi ya kutekeleza azima yao.
Sehemu ya ishirini
Kwenye mazishi, Mama Furaha anaapa kuwa ukweli ni lazima isomwe katika umati huo. Padri James anapingana na mama Furaha kuhusu kuisoma barua hiyo. Mama Furaha anamuonya Padri James kuwa hana la kuficha.
Salimu anatoka katika kundi la watu na kumpora mama Furaha orodha na kuichanachana katika vipande. Mama Furaha anakasirishwa na hilo. Hata hivyo inasomwa barua hiyo ambayo inaelezea mambo yaliyochangia kifo chake na namna kijiji kinachopaswa kuchukua tahadhari na ugonjwa huo kwa kuelezea mambo 10 ili kuepukana na ugonjwa huo.
1. Maudhui
Orodha ni tamthiliya ya tanzia — ramsa ambayo inachambua tatizo la UKIMWI katika sehemu za vijijini katika bara la Afrika. Ni tamthiliya ambayo inajaribu kutumia mazingira halisi ya vijiji vyetu vya kiafrika, mila na desturi za kiafrika ili kuweza kueleza namna ugonjwa huu unavyotafuna maisha ya watu wengi barani Afrika na kwingineko. Mwandishi anajaribu kuonesha umuhimu wa kutambua uzito wa tatizo hili katika mazingira ya kijijini ambalo hawaelewi vizuri kuhusu tatizo hili.
Mwandishi wa tamthiliya anapevuka zaidi katika namna ya kulielezea tatizo ambalo waandishi wengine wamepata kulieleza. Kupitia Furaha na Mama Furaha mwandishi anajaribu kuvunja ukimya na kuamua kueleza mambo ya msingi ya kuzingatia katika mapambano haya ya kutokomeza gonjwa hili hatari la UKIMWI. Mwandishi anaorodhesha mambo hayo kuwa ni:
(a) Matumizi ya Kondomu.
(b) Utoaji wa elimu sahihi.
(c) Uelewa wa tatizo na watu wenye tatizo hill iii kuepuka unyanyapaa.
(d) Uwazi wa kuzungumzia tatizo lenyewe.
(e) Uadilifu wa watu wote katika jamii.
(f) Uwajibikaji kwa jamii nzima kwa nafasi tulizonazo.
(g) Ukweli ill kutuweka huru.
(h) Upendo ndani ya jamii ili kuepusha ukuaji wa tatizo na pia kuwatia moyo waathirika.
(i) Msamaha ni muhimu ili tusihukumu wala kuwa na visasi kwa walioathirika na ambao hawajaathirika.
Kwa ujumla, mwandishi amezungumzia namna watu wanavyopata maambukizi, dalili na hatua za kuchukua ili kupambana na ugonjwa hatari wa UKIMWI.
DHAMIRA ZINAZOJITOKEZA
Dhamira Kuu: Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi
Tamthiliya hii ya Orodha inahusu UGONJWA WA UKIMWI. Mwandishi amekusudia kutoa taarifa muhimu kuhusu ugonjwa hatari wa UKIMWI. Katika utangulizi wake mwandishi anasema: “Wazo langu la msingi lilikuwa kuchunguza mazingira ya msichana wa kijijini anayekufa kwa UKIMWI…, Orodha ni kichekesho na wakati huohuo ni tamthiliya ya kielimu kwa wale wasiojua VVU/UKIMWI.”
Kwa hakika mwandishi anatumia ucheshi kuelezea tanzia kubwa tuliyonayo ndani ya jamii zetu. Tanzia ambayo imeletwa na ugonjwa huu hatari wa UKIMWI. Dhamira hii kuu ya UKIMWI imeelezwa kwa namna ambayo watu wanaelimishwa kuhusu mambo hayo yanaweza kuwekwa katika makundi yafuatayo:
– Ukosefu wa elimu sahihi kuhusu VVU/UKIMWI.
– Umaskini.
– Mmonyoko wa maadili, kutowajibika na kutokuwa waadilifu.
– Kukosekana kwa uwazi, ukweli na upendo.
Mwandishi anaona kuwa mambo hayo, ndio kiini cha tatizo hili la ugonjwa wa UKIMWI. Ili jamii inusurike na janga hili, hatuna budi kuzingatia:
– Ngono salama
– Uadilifu
– aminifu
– Uwajibikaji
– elimu
– Ukweli
– welewa
– Upendo
– uwazi
– Msamaha.
Katika waraka aliouacha Furaha kabla hajaaga dunia anasema,
Kwa kijiji changu kipendwa. Nawashukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope, kwani nadhani maneno haya yanaweza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa nikizidi kuugua. Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika, kukua kama mtu: Hata ninapokuwa nakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna orodha ya vitu ambavyo vilisaidia kuyafupisha maisha yangu, orodha ambayo inaonesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu …..Kondom, uadilifu, elimu,
welewa, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha… ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote…”(uk 44 – 45).
Kwa ujumla, dhamira ambazo zinajenga dhamira kuu ni pamoja na hizi zifuatazo:
(a) Umaskini
(b) Kukosekana kwa elimu/ujinga
(c) Dhana potofu
(d) Mmomonyoko wa maadili
(e) Unafiki
(f) Mapenzi na ndoa
(g) Ukosefu wa huduma za afya
(h) Unyanyapaa
(i) Uwazi wa ukweli
(j) Kukosekana kwa uadilifu na kutowajibika
Kuondolewa kwa mambo hayo hapo juu, kutatusaidia sana katika mapambano yetu dhidi ya tatizo hili la UKIMWI.
(a) Umaskini:
Hii ni hali ya mtu au jamii kukosa uwezo wa kupata uhitaji katika maisha yao ya kila siku. Kwa neno jingine, hufahamika kama `ufukara.’ Katika tamthiliya hii, mwandishi anabainisha kuwa umasikini ni moja ya vyanzo vikuu vinavyofanya wasichana kutumbukia katika mambo yasiyofaa kama ulevi na umalaya. Hivyo, huwa ni vigumu kufanya maamuzi yenye busara ya kujilinda na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Haya yanajitokeza pale Mary anaposema:
“(Akimvuta Furaha kando) Nimekwambia hawa jamaa ni burudani…. hata yule mshamba Juma. Sikia, pata burudani na kuwa mwema, kwa Ecko. Anaweza kukununulia vitu vingi sana! Unadhani wasichana wadogo kijijini hapa wanapataje viatu vipya, magauni na mabegi mapya ili wapendeze… wapendeze kiasi cha kuwavutia vijana wazuri wa kiume?-” (uk. 7 — 8).
Mwandishi anaonesha kuwa jamii ya kijijini sehemu kubwa ina watu wasiojiweza kiuchumi. Kutokana na hilo, wasichana hujirahisisha kwa wanaume wenye pesa ili wapate pesa za kupata mahitaji yao muhimu kama vile nguo, mabegi na viatu vipya.
Mwandishi wanaona kuwa vita dhidi ya UKIMWI iende sambamba na ukombozi wa kiuchumi. Vinginevyo mtu ambaye hajajikomboa kiuchumi huwa na nafasi ndogo sana ya kujilinda na maadui kama maradhi na ujinga.
(b) Kukosekana kwa elimu/ujinga
Elimu ni maarifa yanayomsaidia mtu kupambana na maisha. Mtu asipokuwa na elimu siku zote huwa ni mjinga wa mambo mbalimbali. Mwandishi wa tamthiliya hii ameonesha kuwa kikwazo kingine cha vita dhidi ya ukimwi ni ujinga (kukosekana kwa..elimu). Mwandishi anaona kuwa elimu ya ukimwi inapaswa kutolewa kwa watu wa vijijini. Watu wanapaswa kuelewa ukimwi ni nini? Unaambukizwa kwa njia zipi? Matibabu yake yakoje (dawa za kurefusha maisha)? Mtu anaweza kuepuka vipi? Je, wagonjwa wahudumiwe vipi katika vipindi vyote vya ugonjwa huu, n.k.
Katika kijiji ambacho Furaha alikuwa akiishi inaonekana watu wengi hawafahamu vyema kuhusu Ukimwi. Ukweli wa hoja hii unaweza kuthibitishwa na mazungumzo ya wanakijiji.-
Mwanakijiji wa1: Ndio, lakini katika ofisi ya daktari kaambiwa ana huu ugonjwa wa AIDS!
Mwanakijiji wa 4: Hicho si kitu kizuri
Mwanakijiji wa 1: Wanauita slim kwa sababu ugonjwa wenyewe hukufanya ukondeane.
mwanakijiji wa 3: Lakini anawezaje kuupata ugonjwa kama huo!
Mwanakijiji wa 1: Rahisi! Kuna mtu kamroga…
Mwanakijiji wa 2: Nasikia unaupata kwa kugusa tu!
Mwanakijiji wa 4: Au hata kwa kuiva nao katika chumba kimoja!
Mazungumzo ya wanakijiji hawa yanadhihilisha wanakijiji wengi hawafahamu njia zinazosababisha maambukizo. Wanadhani ugonjwa wa Ukimwi unaambukizwa kwa kurogwa, kugusana na mtu mwenye virusi na kwa njia ya hewa. Haya ni mawazo potofu na yanachangia kuzorotesha mapambano. Ili tuweze kutokomeza gonjwa hili hatari ni lazima wananchi wapewe elimu sahihi na endelevu kuhusu ugonjwa wa ukimwi na virusi vya ukimwi.
(c) Mmomonyoko wa maadili
Hii ni hali ya kuporomoka kwa mwenendo mwema ndani ya jarnii ambapo hutokana na jamii kutokuzingatia mafundisho na maonyo mema katika jamii. Baadhi ya maadili mema ni pamoja na kuepuka kufanya mambo yanayokatazwa na jamii kama vile ulevi, uvutaji wa bangi, uzinzi, uasherati na umalaya.
Mwandishi wa tamthiliva hii anaonesha kutoridhika na namna jamii inavyomomonyoka kimaadili. Mwanclishi anaona kuwa mmomonyoko wa maadili ni chanzo kingine kinachochangia kuenea kwa ukimwi na hivyo kufanya vita hii kuwa ngumu. Kwa mfano; Furaha na Mery wanashindwa kuzingatia mwenendo ulio mwema na badala yake, wanajiingiza katika ulevi na umalaya ambao unapelekeaFuraha kufa kwa UKIMWI. Haya yanaweza kuthibitishwa kutoka katika kitabu
pale baba anapomsura mwanae Furaha;
“Nilichokuwa nafahamu.. hadi sasa Furaha…ni kwamba umekuwa ukitoroka
nyumbani wakati wa usiku wa manane!.. kutoroka… bila ruhusa!.baa… wanaume…
wewe… Malaya usiye na shukurani!” (uk 11).
Mwandishi pia anaona kuwa si wasichana tu ndio hawazingatii maadili mema pia hata watu ambao wameaminiwa na jamii kuwa viongozi wa kusimamia maadili mema. Bila woga mwandishi anabainisha kuwa hata viongozi wa dini sasa wamepoteza mwelekeo na mwenendo mwema. Mfano mzuri ni Padri James.
Badala ya Furaha kuona ametenda dhambi anaamua kwenda kuungama dhambi zake ili arejee katika tabia yake njema. Badala ya kumsaidia kiroho, Padri James anatumia nafasi yake kumrubuni Furaha na kufanya ngono katika chumba cha kusomea. Padri James nasema; (uk. 10).
“Furaha alikuja kama alivyoagizwa na…ee…Ekaristi Takatifu ikapatikana. Lazima uelewe jinsi ilivyo vigumu kwa mtu wa hadhi yangu na wadhifa wangu. Kuna shinikizo kubwa, vishawishi vingi! Kwa watu hawa, mimi ndie padri wao… lakini mimi pia ni mwanadamu! Mahitaji yote haya ya mwanadamu: Peke yangu katika jumuiya hii.
Nafanya kile niwezacho kufanya… na bado, kwangu yaelekea kwamba alikwisha bikiriwa, kwa hiyo ingeleta tofauti gani? Nilidhani pengine hata ningeliweza kumliwaza? Lakini mtu lazima awe mwangalifu… katika jumuiya ndogo namna hii… taarifa husafiri… wakati wowote ……kitu fulani huropokwa”.
Kwa ujumla, kuporomoka kwa maadili katika jamii ni tatizo au kikwazo katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
(d) Mapenzi na ndoa
Hii ni dhamira nyingine ambayo imejadiliwa katika tamthiliya hii ya Orodha. Mwandishi anaona kuwa mapenzi yasiyo ya dhati katika ndoa na katika jamii kwa ujumla ni kikwazo kikubwa kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Mapenzi yasiyo ya dhati hupelekea watu wasiwe waaminifu kwa wenzi wao. Mfano mzuri ni Bw. Ecko. Hakuwa na mapenzi ya dhati kwa mkewe na matokeo yake yeye mwenyewe Bw. Ecko na mkewe wapo katika hatari ya maambukizo ya virusi vya UKIMWI. Mazungumzo ya Bw. Juma na Ecko yanashadidia maelezo haya:
Bw. Ecko: Kwa kweli! Najaribu kukinusuru kijiji hiki kutokana na aibu.
Bw. Juma: Bila kumtaja mkeo!
Bw. Ecko: Nimesema bila kumtaja!
Bw. Juma: Hivyo ndivyo niliyosema. Bila kumtaja! Sasa, hiyo orodha iko mapi?… (uk. 32).
Hofu ya orodha inamfanya Bw. Ecko aisake hiyo barua kwani anajua alishamsaliti mkewe na kwamba hata hiyo orodha alidhani itakuwa na jina lake kama mtajwa au muathirika. Laiti Bw. Ecko angekuwa na mapenzi ya dhati angemlinda mkewe kwa kutoisaliti ndoa yake. Vilevile mapenzi yasiyo ya dhati yamejitokeza kati ya Furaha na Bw. Ecko, Mapenzi yao yaliegemea kwenye pesa na vitu. Furaha alifanyamapenzi na bwana Ecko ili kupata pesa na vitu kama ambavyo rafiki yake, Mary alivvomtanabaisha;
“…kuwa mwema, kwa Ecko. Anaweza kukununulia vitu vingi sana! Unadhani wasichana wanapataje viatu vipya, magauni na mabegi mapya…”
Furaha na wasichana wengi wa kijijini walijali zaidi vitu na fedha badala ya mapenzi ya dhati. Matokeo yake wanaishia kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI na kufanya vita dhidi ya UKIMWI kuwa ngumu zaidi.
(e) Ukosefu wa huduma za afya.
Kijijini maisha ya watu yanapotea kwa sababu huduma za afya zipo mbali sana. Maisha ya waathirika yanahitaji huduma za afya ziwe bora na karibu na pale walipo. Huduma za afya zinazoelezwa hapa ni pamoja na utoaji wa elimu ya afya inayohusu magonjwa hatari kama malaria, kifua kikuu, saratani ya uzazi na UKIMWI, Upimaji wa magonjwa hayo, Matibabu na kuwashirikisha wananchi katika mapambano ya UKIMWI. Huduma hizi zote hazipatikani kwa urahisi kijijini.Haya yanaweza kuthibitishwa na mama Furaha anaposema,
“Kadri muda ulipoendelea, ndiyo Furaha alivyozidi kukondeana,:.. Furaha alikuwa kadhoofika mno hakuweza kuinuka kitandani. Daktarii kutoka mji wa karibu alifika na kuchukua sampuli ya damu ili kupima malaria. Mzee wa kijiji alifika na dawa zake zauganga. Daktari wa mjini alirudi. Alitaka ampeleke Furaha kwenye hospitali ya karibu… “(uk.23).
Hii inathibitisha kuwa kijijini hakuna huduma za afya na hili ni tatizo kubwa katika mpambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI na maradhi mengine ambayo ni nyemelezi.
(f) Uwazi na ukweli
Hii ni dhamira ambayo inajaribu kuonesha umuhimu wa watu kuwa wazi na wa kweli ili kutoa msukumo na mtazamo mpya kuhusu vita hii dhidi ya UKIMWI.
Msanii anaona kuwa umefika wakati wa kuwa wakweli na wawazi kama kweli tuna nia ya kutokomezaUKIMWI. Katika hali ya kejeli, ucheshi anatumia “orodha” ambayo itabaini ukweli. Ukweli upi? Hiki ni kitendawili kinachowasumbua wanakijiji Bw. Ecko, Salim, Juma na Padre wanajaribu kila namna kuona wanaipata orodha hiyo ili kuficha ukweli. Wanadhani ni orodha ya majina ya watu waliotembea na Furaha. Mathalani Padri James anapopinga waziwazi kuhusu kusoma hiyo orodha, mama Furaha anamjibu:
“Hakika, Padri; Wewe huna la kuficha!”
Ingawa mama Furaha anaongea na Padri James lakini matumizi ya wewe yanatugusa sote. Hatuna jambo la kuficha Ni lazima tuvunje ukimya. Tuzungumze mambo yote yanayohusu ugonjwa huu ili kunusuru watu wetu. Siyo ukweli huo tu peke yake, Furaha anapoelewa tatizo linalomsumbua anaamua kueleza ukweli kuhusu tatizo alilonalo. Anaamua kumueleza Salim na wanakijiji wote. .’anasema,
” nina ukimwi, Salim” (uk.29)
Kwa kutaka jamii yake isiangamie, Furaha anaamua kusema ukweli kuhusu mambo yote yajiyochangia kuangamiza maisha yake. Anakuwa muwazi kwa kuandika barua ambayo ndiyo inabeba dhamira kuu ya mchezo huu. Furaha anasema yafuatayo katika barua yake,
“…Kondomu, uaminifu, elimu, welewa, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha… ukosefu wa mambo yote baya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote… wanusuruni watu wetu…wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Muinusuru Afrika… yetu nzuri!”
Ni maneno mazito sana. Furaha anakuwa muwazi na mkweli ili kunusuru jarnii yake na Afrika nzima. Anatambua madhara ya UKIMWI kwa jamii. Haoni sababu ya kuficha. Kwa hakika ukweli huleta uhuru. Ukweli na uwazi utasaidia sana katika mapambano yetu dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.
(g) Kukosekana kwa uadilifu na kutowajibika
Katika jamii kuna watu ambao wanapewa dhamana mbalimbali ili kuiongoza jamii katika nyanja mbalimbali. Watu wenye dhamana wanapaswa kuwa mfano mzuri. Wanategemewa kuiongoza jamii katika njia iliyo sahihi.
Mwandishi anaonekana kukerwa sana namna viongozi na watumishi wengine kutokuwa waadilifu katika nafasi walizopewa ndani ya jamii. Kutokuwa waadilifu kwa jamii zao kunakwamisha,vita ya maadui watatu ambao ni maradhi, umaskini na ujinga.
Mwandishi anamtumia Padri James kama mfano wa watu wasio waadilifu katika jamii. Padri James alipaswa kuwa mstari wa mbele kuwatahadharisha kuacha kuzini, kulewa na maovu mengine badala yake yeye kama Padri anashindwa kutambua nafasi yake katika jamii kwa kujihusisha na mambo machafu kama uasherati. Padri James aliweza kufanya ufuska wake katika nyumba takatifu ya Mungu. Huu ni ukosefu wa maadili. Padri James anasema,
“Furaha alikuja kama alivyoagizwa…ee…Ekaristi takatifu ilipatikana lazima uelewe jinsi ilivyo vigumu kwa mtu wa hadhi yangu na wadhifa wangu”(uk.10).
Baada ya kufanya ufuksa Padri James anaeleza na namna ilivyo ngumu kwa mtu wa wadhifa na hadhi yake kufanya uchafu kama alioufanya. Vita dhidi ya UKIMWI inahitaji watu kuwa waadilifu vinginevyo jamii nzima itaangamia kwa UKIMWI.
(h) Upendo
Hii ni hali ya kuhusudu kitu, mtu kwa moyo wako katika nyakati mbalimbali bila kujali matatizo yatakayojitokeza. Kitu au mtu kuwa ndani ya moyo wako kwa kuwa unakuwa umetoa nafasi hiyo. Upendo ni silaha kubwa sana katika vita hii dhidi ya UKIMWI. Uwepo wa upendo ndani ya jamii utasaidia kulea wagonjwa wa UKIMWI na watoto yatima waliopoteza wazazi wao kwa UKIMWI. Mfano mzuri ni mama Furaha. Huyu ni mtu ambaye alionesha upendo kwa Furaha katika kipindi chote cha ugonjwa wake hadi kumfia mikononi mwake. Haya yanajitokeza katika ukurasa 30.
Furaha:Mimi…mimi sikuwa mtoto mzuri wakati wote, mama.
Mama Furaha: (akicheka). Mimi pia, mwanangu! Hakuna mtu aliye kamili. Lakini uliwaangalia wadogo zako. Na kila mahali ulipokuwapo, kulikuwa na nuru ya jua!
Ulikuwa binti mzuri………binti yangu mzuri…. (Furaha analegea wakati akiongea). Inaelekea kana kwamba umezaliwa Jana tu. Na wakati huo ulizidikufanya nisubiri,
wakati nikiwa na mimba yako. Nakumbuka jinsi ilivyookua, ukikimbia, shambani mwetu, ukijaribu sana kumfurahisha baba yako…unajua, anakujali kwa namna yake…(ananyamaza kidogo wakati akimtazama Furaha ambaye ananyong’onyea mikononi mwake, Analia). Amelala sasa… lala mwanangu.
Upendo wa namna hii unapaswa kuoneshwa kwa wagonjwa wote.
Furaha pia anaonekana kuonesha upendo kwa kijiji chake anapoamua kuandika barua ya wosia ili kuwaepusha watu na ugonjwa huu. Furaha anaanza barua yake kwa kusema;
“Kwa kijiji changu kipendwa” Haya ni meneno ambayo yanaeleza hisia zake kwa kijiji chake.
Anaeleza mambo muhimuya kuzingatia. Anaendelea kusema,
“Ukosefu wa mambo vote haya ndio uloniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote”.
Furaha anamaliza baua yake kwa kusema,
“Wenu awapendae, Furaha.”
Hakika Furaha ni msichana ambaye anaonekana alikuwa na upendo na watu wote kwa kusema,
“Chukueni orodha yangu na muinakili. Ipelekeni kwenye vijiji vingine, miji mingine na
mengine katika hii nchi yetu Wanusuruni watu wetu ili waweze kuyafaidi maisha kikamikfu. Wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Mwinusuru Aftika…Afrikayetu nzuri!”
Ni barua inayobaini upendo na uzalendo kwa nchi yake. Kwa upendo alionao ameamua kuokoa jamii nzima, anapigana vita dhidi ya UKIMWI kwa kutoa elimu kwa jamii. Upendo ni silaha ya kupambana na unyanyapaa na UKIMWI kwa ujumla.
(i) Ulevi
Katika tamthiliya hii ya Orodha, tunaambiwa kuwa ulevi ni tatizo kubwa na ndiyo chanzo kikubwa cha watu kushindwa kujitawala. Msanii anaeleza kuwa watu wanapokuwa wamelewa huwa na maamuzi mabaya ambayo huleta majuto baadaye. Katika kuonesha ulevi ni kikwanzo kikubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI anatuonesha wahusika, Furaha, Bw. Ecko, Bw. Juma na Mery kuwa walikuwa walevi na matokeo yake wakaangukia katika uzinzi na uasherati ambao unaleta majuto makubwa. Hebu tumwone mhusika mkuu jinsi ulevi ulivyomletea matatizo.
Baba: Hakudhamiria nini? Kweli, ulidhani kwamba, ungaliweza kikficha hiyo siri yako ndogo!
Furaha: Siri yangu ndo…unajua pombe?
Baba: Pombe!
Mama Furaha: Pombe!
Furaha: Ndiyo, kule baa!
Mwandishi anaonesha kuwa Furaha alijiingiza katika ulevi na ndivo ikawa chanzo cha yeye kujiingiza katika umalaya ambao unamsababishia kupata ugonjwa wa UKIMWI. Bw. Ecko anathibitisha hill kwa kusema,
“Jambo baya zaidi; Hakika? Tuseme tu kwamba hata tulipofika kwenye ‘chumba changu cha ukapera’ nyumba yangu ya pili tulikuwa tumelewa chakari, hasa!..”
Kwa ujumla ulevi wa aina voyote huwa na madhara makubwa katika mfumo wa ufahamu wa binadamu na matokeo yake ni kushindwa kutoa maamuzi sahihi na kushindwa kujitawala. Mwandishi anaonesha kuwa ni kikwanzo kikubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.
(j) Malezi
Mwandishi anajaribu kuonesha jamii kuwa malezi ni suala ambalo linapaswa kuangaliwa upya. Malezi kwa watoto yanapaswa kuzingatiwa na jamii nzima badala ya kuachia wazazi. Msanii anaonesha namna wazazi wa Furaha walivyojaribu kumlea mtoto wao kwa namna iliyo njema. Furaha alipobadilika mwenendo wake wazazi walimkalisha chini na kumkanya. Kwa mfano. Baba yake Furaha anasema,
“Furaha! Wewe unategemewa kuwaongota watoto hawa. Hawaelekei kufahamu tabia njema hapa nyumbani!”
Hii inaonesha namna ushirikiano unavyotakiwa katika suala zima la malezi ndani ya familia au nje ya familia. Baba anaamua kushirikisha Furaha katika malezi ya wadogo zake. Vilevile, mtoto hakui kwa wazazi wake. Baba anapoona mwenendo wa Furaha pia sio mzuri, anaamua kuongea na mama yake anasema,
Baba: Huyu msichana hatafanikiwa chochote maishani. Nina hakika bado hajafanya aliyopewa shuleni! Siku hizi hata hasaidii shambani kama alivyokuwa akifanya zamani.
Mama: Nafahamu, mpenzi: Hata sijui nifatye nini?… wacha niongee naye….Nadhani yuko katika umri ambao…
Baba: Ni afadhali ufanye hivyo: vinginego, hapa kijijini hakuna mtu atakayetaka kumwoa! Ila tu kwa wale ambao ni washamba wa kule baa!
Hata hivyo malezi ya wazazi na ndugu tu hayatoshi bali jamii nzima inapaswa kushirikiana kuwaweka vijana katika mwenendo ambao unastahili. Mwandishi anaonekana kusikitishwa na tabia ya baadhi ya watu badala ya kusaidia kuelekeza njia sahihi baadhi ya vijana badala yake huwapotosha. Mwandishi anatumia Padri James, Bw. Ecko na Bw Juma kuwa ni mfano mbaya katika jamii kwani wao wameshiriki kuwapotosha na kuwaharibu vijana kama vile Furaha na Mery.
Jamii inapaswa kushirikiana katika malezi ya watoto ill kuwaepusha katika janga hili la ukimwi kwa ujumla.
2. Ujumbe
Ujumbe tunaoupata kutoka kwenye tamthiliya hii ya orodha ni pamoja na:
(i) Asiyesikia la mamaye hufunzwa na ulimwengu. Furaha ni msichana ambaye alikuwa akikaidi ushauri na wazazi wake wote wawili kuwa mwenendo alionao sasa haufai lakini yeye akakaidi. Matokeo yake alijikuta ameambukizwa virusi vya UKIMWI na kumsababishia mateso ya mwili kwa kuumwa muda mrefu hadi mauti yalipomkuta. Tunapaswa kufanyia kazi ushauri muhimu unaohusu maisha yetu kwa ujumla ili kuepuka madhara makubwa.
(ii) Tamaa mbele mauti nyuma. Tamaa za kutaka kupata fedha na vitu mbalimbali harakaharaka vilimtokea puani Furaha. Furaha alishawishika kujiingiza kwenye umalaya ili apate vitu vizuri. Matokeo ya tamaa zake ni kupata ukimwi.
(iii) Ulevi ni chanzo cha matatizo. Furaha alikuwa ni msichana mwenye maadili mema. Mara baada ya kuanza kujiingiza kwenye ulevi ndipo matatizo mengi yalianza kuibuka. Alipewa majina mabaya, alikosana na wazazi na hatimaye kufa kwa UKIMWI.
(iv) Elimu ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya ukimwi. Elimu humkomboa mtu katika giza na kumpeleka katika nuru. Elimu ndogo kuhusu ukimwi ndiyo chanzo cha kushindwa kujikinga na maambukizi. Elimu sahihi ndio njia muhimu ya kuwaokoa watu katika hatari ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na ugonjwa wa UKIMWI.
(v) Kondomu, Uaminifu, uadilifu, ukweli, upendo na uwajibikaji ndiyo mambo muhimu ya msingi ya kuzingatia ili kuiokoa jamii katika janga hili la ugonjwa huu hatari wa UKIMWI
(vi) Umasikini, ulevi, na makundi yasiyofaa ni chanzo cha uchochezi wa uhalifu wa maisha ya vijana kama Furaha hivyo hufanya watu watumbukie katika matatizo makubwa yakiwemo madawa ya kulevya kama ilivyo kwa kitunda na umalaya kama ilivyo kwa Furaha na Mery. Ili tupige vita dhidi ya UKIMWI tunapaswa kupambana na umasikini, ulevi na makundi mabaya katika jamii.
3. Migogoro
Ifuatayo ndiyo migogoro iliyojitokeza katika tamthiliya hii ya orodha:
(i) Mgogoro kati ya mama Furaha na Padri James kuhusu kusoma orodha aliyoandika Furaha. Padri James anampinga mama Furaha kusoma orodha hiyo. Mama Furaha anamuonya Padri James kuwa hana cha kuficha hivyo aliisoma hiyo barua kwa nguvu. (uk. 3 na 43).
(ii) Mgogoro kati ya Furaha na dada mdogo. Katika harakati za kutoroka usiku kwenda baa. Dada mdogo hapendenzwi na tabia hiyo na kumtishia kumsemea kwa mama yao. Mvutano huo unaisha kwa Furaha kumtishia kumchinja mdogo ikiwa atatimiza azma yake ya kumsemea kwa mama. (uk.6)
(iii) Mgogoro kati ya Baba na Furaha kuhusu kutoroka bila ya ruhusa ya wazazi na Pia kujihusisha na ulevi na umalaya. Suluhisho la mgogoro huu ni baba kumpiga mwanae na kumuonya kwa maneno makali. (uk.10 — 12).
(iv) Mgogoro kati ya mama Furaha na Salim kuhusu orodha. Salim hakubaliani na uamuzi wa mama Furaha na kulazimika kupora orodha na kuichana vipande. Suluhisho ni mama Furaha kunikumbusha fadhila za Furaha kwa Salim nakuamua kusoma karatasi iliyobaki na kuokota vipande vile na kuviunganisha na kusoma orodha. (uk. 43-44).
(v) Mgogoro kati ya Salim na Furaha kuhusu orodha. Salim analazimishwa apewe orodha hiyo aisome kwanza lakini Furaha anakataa na kumueleza kuwa itabidi asubiri. Wanarushiana maneno yenye visa hadi mama Furaha anaingia na kuamuru Salim atoke nje na aaende zake.
(vi) Mgogoro wa kinjisia uliomo ndani ya Salim, Ecko, Padri James na Juma. Kila mmoja alitembea na Furaha na wanasikia kuna orodha wanaingiwa na hofu ya majina yao kuwepo au kuambukizwa UKIMWI. Kila mmoja anaamua kuondoa hofu hiyo kwa kwenda kuisaka orodha hiyo bila mafanikio. Wanajaribu kuleta hila iii isisomwe lakini wanashindwa. Inaposomwa wanagundua haikuwa orodha ya majina yao. (uk. 31-45).
4.
Msimamo wa mwandishi
Mwandishi wa tamthiliya ya Orodha anamsirnamo wa kiyakinifu. Amechambua ugonjwa wa ukimwi kwa jicho la kipembuzi bila ya kuficha jambo. Amejadili mitazamo ya watu wa kijiji kuhusu ufahamu wao kuhusu ukimwi na changamoto mbalimbali zilizopo katika nchi zinazoendelea hususani nchi za kiafrika kuhusu suala zima la UKIMWI.
Mwandishi amebainisha kuwa ukosefu wa konndomu vijijini, uadilifu, Elimu, uelewa, uwazi, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha ndiyo huchangia vifo vya watu wengi. Vilevile mwandishi anaona kuwa ufuatiliaji wa mambo haya na usambazaji wa mambo haya sehemu mbalimbali ndio itakuwa njia sahihi za kutokomeza ukimwi na madhara yake kwa ujumla. Anasema ujumbe huu ndiyo iwe barua kwa wote ili kuokoa kizazi hiki.
5.
Falsafa ya mwandishi
Mwandishi wa tamthiliya hii anaelekea kuamini kuwa ukweli, uwazi na uadilifu ni mambo muhimu sana katika jamii inayotishiwa na majanga makubwa kama ya UKIMWI. Sehemu kubwa ya wahusika amewaumba kwa namna ya kuonyesha namna ya kukabili ukweli na kuwa wazi. Wapo wahusika wamefanikiwa kwa hilo akiwemo Furaha na mama Furaha, wapo wahusika wanaoshindwa au kuwa na hofu. Mfano. Bw. Ecko, Salim na Bwana Juma.
6. Fani
(a) Muundo
Mwandishi wa tamthiliya ya orodha ameweza kuweka kazi yake yote katika onyesho moja. Onyesho hili lina jumla ya sehemu ishirini (uk. 20).
Mpangilio wa visa na matukio kwa ujumla ni changamano. Sehemu ya kwanza na ya pili inazungumzia matukio ya siku ya mazishi ya Furaha. Sehemu ya tatu hadi ya kumi na sita (16) inazungumzia maisha ya Furaha hadi kifo chake. Sehemu ya 17 hadi 19 inahusu mzozo wa uwepo wa orodha aliyoandika Furaha enzi za uhai wake. Sehemu hizi zinazungumzia harakati za kuitafuta barua hiyo kwa udi na uvumba bila mafanikio. Sehemu ya ishirini inahusu mazishi na usomaji wa barua yenye orodha na na mchezo unaishia hapo.
Kwa ufupi muundo ni changamano kwa kuwa sehemu ya 1-2 ni mazishi na 3-20 ni moja kwa moja yaani mwandishi kaanza na kifo cha Furaha sehemu ya kwanza na pili halafu maisha ya Furaha hadi kifo na mazishi yamejitokeza kwa mtiririko wa moja kwa moja kuanzia sehemu ya 3-20.
(b) Mtindo
Mtindo ambao umetumika ni dayolojia. Mwandishi ametumia mtindo wa majibizano kwa kiasi kikubwa katika kazi yake. Ni sehemu chache sana mwandishi ametumia monolojia (uk. 10) Padri James nasema;
“Furaha alikuja kama alivyoagizwa na………ee.. Ekaristi takatifu ilipakana. Lazima uelewe jinsi ilivyo vigumu kwa mtu wa hadhi yangu na wadhifa wangu. Kuna shinikizo
kubwa, vishawishi vingi! Kwa watu hawa, mimi ndiye Padri wao… lakini mimi pia ni mwanadamu! Mahitaji yote haya ya mwanadamu peke yangu katika jumuiya hii.
Nafanya kile niwezacho kufanya… na bado, kwangu,yaelekea kwamba…”
Huu ni mfano to wa matumizi ya monolojia. Padri James alikuwa akizungumza peke yake kabla ya kuondoka. Sehemu nyingine ambazo mwandishi ametumia monolojia ni uk 23, 37, 39, 40, n.k. Kuna matumizi ya barua ambayo ndiyo imebeba ujumbe wa mwandishi. Barua hiyo inapatikana(uk. 44 — 45). Barua yenyewe inasomeka hivi;
“Kwa kijiji changu kipendwa;
Nawashukuru kwa kufika kwenu na kuyasikiliza maneno yangu ya mwisho. Msiogope, kwani nadhani maneno haya yanameza kuwasaidia. Katika hii miezi ya mwisho nimelala kitandani nikifa, nikizidi kuugua.
Nilipata muda mwingi wa kufikiri, kubadilika, kukua kama mtu; hata ninapokuwa nakufa. Katika ukurasa unaofuata kuna orodha ya vitu ambago vilisaidia kuyafupisha maisha yangu. Orodha ambayo inaonyesha kwenu nyote ukweli juu ya kifo changu. Mama tafadhali wasomee watu wote orodha hii.
Uepukaji
Uaminfu
Elimu
Welewa
Uwazi
Uadilifu
Uwajibikaji
Ukweli
Upendo
Msamaha
Ukosefu wa mambo yote haya ndio ulioniua. Ufuatiliaji wa mambo yote haya unaweza kuwaokoa ninyi nyote. Chukueni orodha yangu na muinakili. Ipelekeni kwenye vijiji vingine, miji mingine na majiji mengine katika hii nchi yetu nzuri. Wanusuruni watoto wetu ili wasiwe yatima. Muinusuru Afrika….Afrika yetu nzuri!
Kwa kijiji changu, kiishi maisha marefu na kiwe na furaha! Msinihukumu mapema mno. Kwa mama, baba na ndugu zangu nawapenda. Jaribuni kuwa wenye furaha na muishi maisha ya furaha wakati mnaweza kufanya hivyo!
Wenu awapendaye, Furaha”.
Matumizi ya barua hii katika tamthiliya unaleta athari kubwa sana kwani ni kumbukumbu tosha na ni wosia kwa watu wote ili kuwaepusho na ukimwi. Mwandishi ametumia nafasi zote tatu. Nafsi ya pili imetawala sana kwa sababu mwandishi ametumia mtindo wa dayolojia.
Mifano:
(i) Nafsi ya II
Mama Furaha: Unathubutuje, Salim?… (uk.44).
(ii) Nafsi ya III
Mama Furaha;… Kabla hajafa alitaka nimwahidi kumfanyia kitu Fulani; Hapo kwenye mazishi. Ingawaje alikuwa na maumivu na mateso… (uk. 43).
(iii) Nafsi ya I
Salim: nilikuwa na shughuli nyingi…….Nikijijenga katika kazi yangu mpya ya ualimu… na sikuwa na muda wa kumwona Furaha kwa muda… (uk.27).
Pia mwandishi ametumia mtindo wa lugha ya mtaani ili kuakisi lugha ya watu wa mtaani, kijiweni na lugha ya mateja.
Mfano:
Kitunda: Mshikaji, poa! Unaweza kuniamini: tunaweza kutazama picha, kusikiliza muziki ….unaweza hata kuvuta ganja langu kidogo, mwanangu.
Furaha: Kuvuta nini lako…? (Anarudi nyuma)
Kitunda: Mezea, mtoto, lazima ujifune lugha za mitaani vinginevyo Dar kutakuwa noma tu! Mwanangu! Ni kwamba unaweza kujaribu majani… manjuani! (uk. 14).
(c)
Wahusika
Mwandishi ameweza kuumba wahusika ambao wameweza kudhibiti nafasi zao. Wahusika ambao amewatumia ni Furaha, Mama Furaha, Baba, Mary, Bw. Chaka, Ecko, Bw. Juma, Padri James, Kitunda, Salim, Wanakijiji, Daktari na Dada mdogo.
Wasifu wa wahusika katika tamthiliya ya Orodha
(i) Furaha
- Huyu ni msichana wa mri wa kati ya miaka 13-19.
- Ndiye mhusika mkuu katika tamthiliya hii.
- Ni msichana asiye na msimamo thabiti kwani aliweza kuyumbishwa kwa urahisi na Mary.
- Ni muathirika wa ugonjwa wa UKIMWI.
- Ni mkweli.
- Ni muwazi.
- Ni malaya.
- Ni mlevi.
edu.uptymez.com
Mhusika huyu anafaa kuigwa kwa uwazi na ukweli kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.
Hafai kuigwa kuhusu tabia ya umalaya na ulevi.
(ii) Mama Furaha
- Huyu ni mama mzazi wa Furaha.
- Ni mchapakazi.
- Ni mpole.
- Ni mama mwenye upendo.
- Ni mkweli.
- Ni muwazi.
- Ana msimamo.
edu.uptymez.com
Anafaa kuigwa katika jamii kwani ni mama asiyetetereka katika ulezi wa watoto na familia nzima.
(iii) Baba
- Ni baba mzazi wa Furaha.
- Ni mkali.
- Ana upendo.
edu.uptymez.com
Ana lugha kali kwa wanawe
(iv) Mary
- Ni msichana.
- Ni rafiki yake Furaha.
- Ni malaya.
- Ni mlevi.
edu.uptymez.com
Hafai kuigwa na jamii.
(v) Bw. Ecko
- Ni mwanaume mtu mzima.
- Ni mfanyabiashara.
- Ni mlevi.
- Ni mzinzi.
- Si muadilifu au mwaminifu kwenye ndoa yake.
- Anatamaa.
- Ni muathirika wa ukimwi.
edu.uptymez.com
Hafai kuigwa na katika jamii.
(vi) Bw. Juma
- Ni mwanaume mtu mzima.
- Ni rafiki yake Bw. Ecko.
- Ni mlevi.
- Ni mzinzi.
- Ni mtu mwenye tama.
- Ana lugha chafu.
edu.uptymez.com
Hafai kuigwa na jamii.
(vii) Padri James
- Ni mtumishi wa Mungu katika kanisa la katoliki.
- Ana cheo cha upadri.
- Si muadilifu.
- Ni dhaifu kwa wanawake.
- Anaweza kuwa muathirika wa UKIMWI.
- Si mkweli.
edu.uptymez.com
Hafai kuigwa na
(viii) Kitunda
- Ni kijana wa mtaani.
- Ni mlevi.
- Ni mvuta bangi.
- Ni mhuni.
- Ana lugha ya kihuni.
edu.uptymez.com
(ix) Salim
- Ni kijana wa kiume.
- Ni rafiki wa kiume wa Furaha.
- Ni msomi.
- Anaweza kuwa muathirika wa UKIMWI japokuwa alitumia Kondomu baadhi ya siku alizokutana na Furaha.
- Si mtu adilifu.
- Si muwazi.
- Si mkweli.
edu.uptymez.com
(x) Wanakijiji 1-3
- Ni wanakijiji wa kijijii cha akina Furaha.
- Ni majirani wa wahusika wengine.
- Ni marafiki wa Kitunda.
- Ni watu wasiokuwa na ufahamu kuhusu UKIMWI.
- Wana dhana potofu.
- Ni wambea.
edu.uptymez.com
(xi) Dada mdogo
- Huyu ni ndugu wa kike wa Furaha.
- Ni mdogo kwa umri.
- Ni mwoga.
- Hapandezwi na nyendo za dada yake.
edu.uptymez.com
(xii) Daktari
- Ni mtaalamu wa afya kutoka mjini.
- Ndiye alichukua sampli ya damu.
- Ni mchapa kazi.
edu.uptymez.com
Uainishaji wa Wahusika katika tamthiliya ya Orodha.
Wahusika katika tamthiliya ya Orodha wamegawanyika katika ma kundi makuu matatu:
(a) Wahusika wakuu.
(b) Wahusika wasaidizi au wadogo.
(c) Wahusika wajenzi.
Katika tamthiliya ya Orodha ina mhusika mkuu mmoja tu ambaye ni Furaha. Huyu ndiye anayejitokeza toka sehemu ya 1-20. Mhusika huyu ndiye kabeba dhamira kuu ya mchezo huu. Dhamira kuu ni UKIMWI na ni mhusika pekee aliyekufa kwa UKIMWI.
Wahusika wasaidizi ni: Mama Furaha, Bw. Ecko, Bw. Juma, Padri James, Mary, Salimu, Baba na Kitunda. Hawa ni wahusika ambao wametumika kumjenga mhusika mkuu. Wahusika hawa wamebeba dhamira ndogondogo zisizojenga dhamira kuu.
Kwa mfano:
(i) Mama Furaha – dhamira ya upendo, ukweli na uwazi
(ii) Padri James – uadilifu na Uwajibikaji
(iii) Salim – elimu
(iv) Bw.Ecko, Bw. Juma – ulevi, uaminifu, n.k.
Wahusika wajenzi ni Dada mdogo, Daktari na Mzee wa kijiji wahusika hawa wamejitokeza ama mara moja au wametajwa tu. Ukiondoa Dada mdogo ambaye amejitokeza kama mara mbili katika ukurasa wa 5 na 6 wahusika wengine wametajwa tu na wahusika wengine ukurasa wa 23, 24 na 25.
(d) Matumizi ya Lugha
Lugha iliyotumika ni ya kawaida, inaeleweka na imeshahenezwa kwa kiasi fulani tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.
(i) Misemo/Nahau
Misemo/ iliyotumika katika tamthiliya hii ni kama ifuatayo:
– “Shuga dadi “… (uk. 6) unamaanisha wanaume wenye umri mkubwa wanaopenda kutembea (kufanya mahusiano ya kimapenzi na wasichana wadogo wa umri wa binti zao).
– “Mshamba”…. ark. 7) ni mtu ambaye hajui mambo mengi ya mjini au mambo ya kileo.
– Furaha anavuna mbegu ya kifo aliyoipanda…..(uk. 27). Kuvuna mbegu ni msemo unaomaanisha kupata kitu kutokana na matendo uliyotenda. Ni msemo unatokana na msemo usemao “Utavuna ulichopanda”.
(ii) Misimu
Mwandishi ametumia lugha ya misimu kuweza kutambulisha mhusika. Misimu iliyotumika ni ile ya mtaani au misimu ya vijana katika vijiwe. Lugha hii imtumika (uk. 12-14). ni mazungumzo ya kitunda na Furaha.
Mifano ya misimu:
– Mshikaji — (uk 12, 13, 14)
– Bomba mchizi — (uk .13)
– Poa — (uk. 14)
– Ganja — (uk. 14)
– Majani — (uk. 14)
– Nitakulinda — (uk.14)
– Mwanangu — (uk. 14)
– Kuvinjari— (uk.14)
Haya ni maneno yanayotumika mtaani, hususani hutumiwa na vijana wa vijiweni katika miji. Maneno hayo yana maana zifuatazo:
(i) Mshikaji — rafiki au jamaa
(ii) Bomba mchizi — sawa rafiki au ndugu
(iii) Poa — vizuri au sawa
(iv) Ganja, majani – bangi
(v) Nitakulinda – nitakusaidia
(vi) Mwanamgu — mtu wa karibu au rafiki yangu
(vii) Kuvinjari — kuzunguka au kutalii
(iii) Tamathali za Semi
Tashibiha:
Katika tamthiliya hii ya Orodha mwandishi ametumia tashibiha chache. Tashibiha zilizotumika ni kama zifuatazo:
“Yeye ni kama punda wa kijiji…” (uk 18)
Mwanakijiji wa 1 alikuwa anamfananisha Furaha kuwa yuko sawa na punda ambaye kila mtu alimpanda. Tashibiha imetumika pia (uk.13) pale kitunda anapojaribu kulinganisha jiji la Dsm na lile la New York. Anasema,
“Kisura, ni kama jiji la New York”
Mfano mwingine wa tashibiha unapatikana (uk. 43) mwandishi anaposema,…”vipande vinaanguka kama theluji.”
Sitiari
Sitiari nazo zinatumika kwa kiasi fulani kwa mfano: Baba anaposema, ” nyie, mbu wadogo ….”(uk 4, 10)
Baba anawafananisha watoto wake na mbu wanaonyonya damu
Mubalaagha
Katika uandishi wake kuna maelezo ambayo mwandishi anaonekana kutia chumvi.
Kwa mfano:
“Furaha: sijui unachokiongea. Nani aliyesema mambo hayo?
Mama Furaha: Nusu ya kijiji kizima….”
Mama Furaha alipaswa kusema wengi badala yake anatia chumvi kuwa ameambiwa na watu karibu nusu ya kijiji.
Kijembe na Kejeli
Kejeli na vijembe vimejitokeza katika tamthiliya hii, mwandishi ametumia kuonesha bezo la dhana fulani.
“Nieleze waewe. We ni mzee wa kutosha kuwa baba yangu!” (uk. 7)
“Inafurahisha kuona hufikiri i wewe mwenyewe tu.” (uk 41)
Bw. Juma alitoa kejeli hii kwa Bw. Ecko ambaye ni mbinafsi.
Tafsida
Kuna matumizi ya tungo ambazo zimesaidia kuficha makali ya maneno. Tafsida zimetumika sehemu kubwa ya tamthiliya. Mwandishi anaonekana kuelewa utamaduni wa Waswahili kuwa kuna baadhi ya maneno hayatajwi hadharani.
Kwa mfano:
Mary: Hiyo ni bia yake ya mwanzo
Furaha: Ni chungu
Mary: Ladha yake utaizoea tu!
Bw. Juma: Kama ulivyozoea wewe, mayai yangu madogo!
Bw. Ecko:Unaona! Inashangaza jinsi ambavyo mtu unaizoea haraka ladha hiyo! Bw.Juma (Kwa Mary): Kama ulivyofanya wewe, mishikakiyangu
midogo…..(uk. 7)
Bw. Juma anapotaja “Mayai yake madogo” na “Mishikaki midogo” anamaanisha sehemu zake za siri. Mifano mingine ya tafsida kutoka katika tamthiliya hii ni pamoja na:
(iv) Mbinu nyingine za Kisanaa
Mdokezo:
Kwa mfano:
– Furaha……….. fur……….. tuta…………. (uk. 9)
– Ndiyo, padri…. Ni……. (uk. 8)
– Misamaha, padri: Mi (uk. 36)
…kuendelea na….. (uk. 39)
– Uepukaji………… (uk. 44)
Mbinu hii imetumika kwa kiasi kikubwa sana katika tamthiliya hii ya Orodha. Mwandishi amekuwa akianza neno au maneno na kuyacha bila kumalizia.
Takriri
Kumekuwa na hali ya kurudiarudia, maneno au sentensi katika tamthiliya hii. Mwandishi ametumia mbinu hii kwa lengo la kuonesha msisitizo. Kwa mfano: Padri James: ….. Hili ni jambo zito sana….. sanasana….. sana hasa….(uk. 9).
Mwanakijiji wa 2: Kondom
Mwanakijiji wa 3: Elimu
Mwanakijiji wa 4: Welewa
Mwanakijiji wa 1: Uwazi
Kitunda: Uadilifu
Padri James: Ukweli
Mary: Upendo
Salimu: Msamaha …….. (uk. 44).
Maneno haya yamejirudia tena (uk. 45) kwa mtiririko uleule na wahusika wale wale.
Tanakali Sauti:
Mwandishi ametumia miigo ya sauti ili kuonesha uhalisia na hisia za wahusika.
Kwa mfano:
(a) Myaau! — ( uk 33 — 34).
(b) Oooowww! — (uk . 35).
(c) Owww!……….. (uk. 35).
(v) Picha na Taswira
Mwandishi ametumia lugha ya picha. Mfano mzuri ni matumizi ya neno “Mbu” Baba anaposema, “Karibu nitakufa njaa hali nyie mbu wadogo mwainyonya damu yangu yote?” (uk. 4).
“Mbu” ni neno lililotumika kuleta taswira ya utegemezi kwa njia ya kunyonya damu.
(e) Mandhari
Mandhari iliyotumika katika tamthiliya hii ni ya kijijini vijiji vilivyotumika ni vile vya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Matukio yametokea katika viunga na barabara za vijijini, sehemu za baa na nyumbani. Kwa ujumla mwandishi ametumia mazingira ya vijijini ambako watu hawajapata elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.
(f) Jina la Kitabu
Orodha ni jina la kitabu ambacho kimetafsiriwa katika “The List” ambapo iliandikwa kwa kiingeraza. Orodha ni jina la kitabu ambalo linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu. Ndani ya kitabu mhusika mkuu Furaha kabla ya kifo aliacha barua yenye orodha ya mambo muhimu ya kuzingatia ili kuiokoa jamii nzima kutokana na habari ya kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI. Orodha inayowachanganya watu kijijini kwani walidhani ni Orodha ya majina ya watu ambao walitembea (fanya mapenzi) na Furaha. Ni kichekesho chenye mafunzo, mambo yanayoorodheshwa ndiyo msingi wa dhamira mbali mbali zinazojenga dhamira kuu ya UKIMWI. Orodha yenyewe ni kondom, uaminifu, elimu, welewa, uwazi, uadilifu, uwajibikaji, ukweli, upendo na msamaha.
Kwa hiyo jina la kitabu linasadifU yaliyomo katika kitabu kwani ndani ya kitabu kuna “Orodha” inavyoweza kuokoa jamii katika janga la ugonjwa wa UKIMWI.
KUFAULU NA KUTOFAULU
Kufaulu kwa Mwandishi
Mwandishi amefaulu kufikisha ujumbe wake kwa walengwa. Mwandishi ameweza kujadili vyema tatizo la UKIMWI kwa kutumia mazingira ya kijijni. Mwandishi ameeleza wasiwasi wake kuhusu uelewa wa watu waishio kijijini kuhusu ugonjwa wa UKIMWI. Lakini pia ameweza kueleza mambo ya msingi ya kuzingatia katika mapambano kwa kutumia mbinu ya waraka (barua) (yenye orodha ya mambo hayo muhimu kuzingatia). Barua ile inatumika kama wosia ambao unasomwa siku ya mazishi. Siku yenye huzuni na hofu mioyoni mwa watu ili kuleta athari ya hofu na woga kuhusu UKIMWI.
Anatumia wahusika wachache ambao hawamchanganyi msomaji. Wahusika wa rika na jinsia mbalimbali wametumika kuwasilisha mawazo ya watu mbalimbali kuhusu UKIMWI.
Kutokana na uzito wa tatizo linalojadiliwa, mwandishi amefaulu kutumia lugha inayoeleweka kwa urahisi iliyojaa ucheshi ikinyunyiziwa tamathali za semi na mbinu mbalimbali za kisanaa. Vilevile mwandishi amekuwa makini kujali utamaduni wa jamii husika kwa kutotumia lugha ya matusi na badala yake ametumia tafsida kulinda miiko ya utamaduni wetu katika kutumia lugha.
Mwandishi amefaulu pia kupangilia matukio kutokana na ukubwa wa tatizo linalozungumziwa. Mwandishi anaanza na msiba kuonyesha kuwa jambo lililopo mbele yetu ni msiba wa jamii na anamaliza sehemu ya mwisho kwa msiba kuonesha msisitizo wa dhamira kuu.
Kwa ujumla, mwandishi amefaulu kifani na kimaudhui kufikisha ujumbe aliokusudia kwa jamii.
Kutofaulu kwa Mwandishi
Mwandishi ameshindwa kueleza njia mbalimbali zinazoeneza UKIMWI. Toka mwanzo hadi mwisho wa kitabu mwandishi ameonesha njia moja tu ambayo ni kufanya mapenzi yasiyo salama. Hii ni muhimu ili kupunguza unyanyapaa.
Mwandishi ameshindwa kugawa kitabu katika maonyesho mbali mbali. Kitabu kizima kina onesha moja lenye sehemu ishirini. Mwandishi angeweza kuweka sehemu 20 katika maonesho matatu. Hii ingeweza kusaidia kufuatilia matukio kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa.