Form 4 Kiswahili – VITABU TEULE VYA FASIHI

Share this post on:

 

UHAKIKI WA USHAIRI Jina la kitabu: WASAKATONGE
Mwandishi: MOHAMED .S. KHATIBU
Wachapishaji: OUP (T) Ltd
Mwaka: 2003

Utangulizi
Wasakatonge ni diwani yenye mashairi yanayotetea wavujajasho wanaonyanyaswa, kuonewa, kudharauliwa na kunyonywa na wenye navyo. Ni diwani inaoonyesha uozo wa jamii na athari zake kwa wanyonge. Diwani hii ni chachu ya kuzindua umma unaonyanyaswa ili udai haki yao dhidi ya wanasiasa madikteta wanaotumia nguvu za dola kwa maslahi yao.

Maudhui
Dhamira kuu

 (i) Ujenzi wa jamii mpya

 (ii) Ukombozi

  Ujenzi wa jamii mpya
Mwandishi anajadili Kwa kiasi kikubwa suala la ujenzi wa jamii mpya. Jamii ambayo itatupilia mbali uonevu, unyonyaji, dhuluma unafiki, usaliti, uongozi mbaya, matabaka, ukasuku na hali ngumu ya maisha. Jamii ambayo hatamu zote za utawala, uchumi na siasa zitakuwa katika misingi ya usawa na haki.

      Kama anavyoonesha kwenye diwani yake ya Fungate ya Uhuru kuwa suala la ujenzi wa jamii lilianza mara baada ya uhuru na kuimarishwa na kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967. Katika diwani hii msanii anaonyesha kuwa bado hatujafanikiwa kujenga jamii hiyo kutokana na sababu zifuatazo.

    Kwanza katika jamii yetu bado kuna msuguano mkali sana wa kitabaka kati ya tabaka tawala la wenyenavyo linalonyonya na kuligandamiza tabaka la chini la makabwela. Shairi la “Kansa” na mengine kama vile “Wasakatonge”,
“Asali” na “Mumiani” ni ushahidi wa kutosha unaobainisha vurugu katika jamii.

     Pili hali ya udikteta, unafiki na usaliti uliokithiri katika nchi zetu umeoneshwa katika diwani hii. Msanii anajadili masuala haya kwa kuonesha jinsi viongozi wa nchi na dini wanavyosaliti wananchi na waumini wao. Haya yanajionesha wazi katika mashairi ya “Wasodhambi” (uk. 14), “Pepo bila kifo” (uk.14), “Uasi” (uk. 8). “Madikteta” (uk.21) na “Nahodha” (uk. 41).

     Suala la uongozi mbaya nalo linaoneshwa na msanii katika diwani hii. Msanii anaona bado kuna uongozi mbovu katika jamii yetu katika mashairi ya “Tonge la Ugali” (uk. 20), “Madikteta” (uk.21), “Fahali ya Dunia” (uk. 45-46), “Vinyago” (uk. 49) na “Nahodha” (uk. 41-42).

     Ni kutokana na matatizo hayo na mengineyo, ndio maana msanii anonesha kuwa tumeshindwa kujenga jamii mpya. Katika kujadili dhamira hii ya ujenzi wa jamii mpya, Mwandishi ameonesha mbinu mbalimbali zinazoweza kutumiwa na jamii katika zoezi hilo. Mbinu hizo ni kama vile:

 (i) Kupiga vita uongozi mbaya

 Msanii anaonesha kuwa oungozi mbaya ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya. Suala la uongozi mbaya linaonekana kuwa tatizo sugu katika nchi nyingi za Kiafrika na kama halitatafutiwa tiba basi tutaendelea kuwa na machafuko ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kila siku. Mwandishi amelionesha suala hili katika shairi la “Madikteta” (uk. 21) na “Unyama” (uk . 47). Kwani viongozi wengi huongoza nchi Kwa mabavu na sio kwa kufuata sheria zilizowekwa na nchi husika. Kwa sababu ya uchu wa madaraka, wengi huingia madarakani kwa mtutu wa bunduki.

    Vilevle katika shairi la “Miamba” (uk.27) ambalo ameonesha kwa kutumia taswira kwa kuonesha “mbugha” kama nchi na “simba na chui” kama viongozi wa nchi, anaonesha kwamba viongozi wa nchi ndio wanaomiliki vitu vya muhimu (njia kuu za uzalishaji mali) na walio wengi hawamiliki chochote na matokeo yake ni kunyonywa na viongozi hao. Pia shairi “Mtafaruku” (uk.36) ameonesha jinsi viongozi wanaovyowanyima watu wa kawaida uhuru wa kusema au kuzungumzia maovu yaliyomo katika jamii yao.

    Katika shairi la “Nahodha” (uk. 41).  Anaonesha kuwa baadhi ya viongozi hushindwa kuongoza nchi zao na wanapoambiwa kujiuzulu na wananchi huwa hawakubali na shairi la “Peponi bila kifo” (uk. 14) ameonesha tabia ya baadhi ya viongozi kuishi maisha ya raha na ya anasa wakati hawawajibiki. Ni vigumu katika uhalisia kwenda peponi bila kupitia kufa kama mshairi anavyoelezea, huwezi kupata pepo bila kupitia kifo. Hii ni lugha ya picha anayotumia msanii kuonesha kifo ni kama mapambano, ili kupitia daraja la mafanikio ambayo ni pepo kulingana na maelezo ya mwandishi.
Pia katika mashairi ya “Tonge la ugali” (uk. 20),  “Fahali ya Dunia” (uk.45), “Vinyago” (uk. 49) yanaonesha uongozi mbaya katika jamii. Hivyo ili tuweze kujenga jamii mpya lazima tupige vita uongozi mbaya.

 (ii) Kuwa na demokrasia ya kweli na utu.

  Katika dunia yetu ya sasa, demokrasia na utu vimetoweka na kupotea kwani katika nchi nyingi zinazofuata mfumo wa kidemokrasia huwa si demokrasia ya kweli. katika nchi ya kidemokrasia wananchi wanakuwa na uwezo wa kupinga au kukataa yale yanayokuwa kinyume na watakavyo.

     Katika diwani hii, msanii ameonesha kuwa katika jamii yetu hakuna demokrasia ya kweli na kunapokosekana demokrasia ya kweli hata utu hupotea. Haya yanajidhihirisha wazi katika mashairi ya “Madikteta” “Saddam Hussein” (uk. 26-27)  na “Unyama” (uk. 47-48).

     Katika mashairi haya ameelezea juu ya viongozi ambao huongoza nchi bila bila kujali utu Kwa kuwafanyia raia wao mambo ambayo huwa ni kinyume na misingi ya ubinadamu. Kama demokrasia inavyojieleza yenyewe, hujali zaidi utu wa  mtu, hivyo ni vizuri viongozi waongozapo wasijali utu wao tu, bali ajali nawale wanaowaongoza. Hivyo, ili tujenge jamii mpya lazima tuwe na demokrasia ya kweli.

(iii) Kupiga vita ukoloni mamboleo

 Ukoloni mamboleo unaonekana ni kikwazo kikubwa cha ujenzi wa jamii hapa nchini. Mshairi ananitaka jamii kupiga vita ukoloni mamboleo Kwani unaathiri jamii nzima katika suala zima la maendeleo katika nyanja zote muhimu ambazo ni uchumi, siasa na utamaduni kwa ujmla.

 Katika shairi la “Hatua Kali” (uk.8-9) anaonesha kuwa uchumi wa taifa letu bado una tegemea misaada toka nje, mfano mitaji, madawa, mashine na pembejeo nahii ndio inayotufanya tudumae na tuwe tegemezi. Mshairi anaonesha athari za ukoloni mamboleo katika shairi la “Wafadhiliwa” (uk38) kuwa viongozi wa nchi wanakuwa ni watekelezaji wa magizo kutoka wa wahisani ambao huwa wanajali maslahi yao zaidi. Matokeo yake ni kwamba nchi inafadhiliwa hukosa uhure wa kujiamulia mambo yao kutokana kulaziamishwa kutimiza yale tu yanayotakiwa na wahisani hao.

Katika shairi la “Tiba Isiyobu” (uk. 18), anaonesha jinsi misaada inayotolewa na wahisani inavyokuwa na masharti magumu. Masharti haya yanapelekea kutawaliwa kwa nchi hiyo kiuchumi na nchi inayotoa misaada pindi washindwapo kulipa madeni au kutimiza masharti yao, yaani kutawaliwa kwa kufuata maagizo yao. Kwa hiyo, msanii anaitaka jamii iwe makini na misaada toka kwa wahisani.

Katika shairi la “Klabu” (uk.50) anaonesha kuwa utegemezi na kuombaomba misaada hujenga mazingira mazuri ya nchi kwa kuvamiwa na nchi za kibepari. Hivyo msanii anaonesha kuwa ili tuondokane na ukoloni mamboleo tusiwe tegemezi, bali tuchape kazi kwa kuendeleza viwanda vyetu ili kukuza uchumi wetu, tupige vita rushwa, tuache kuombaomba hovyo.

 Msanii anaendelea kuiasa jamii kuwa hakuna msaada unaotolewa bure bila ya mtoaji kujua nini atafaidika na msaada huo. Hivyo nchi inaposaidia nchi nyingine, lazima imeona faida mahali hapo ya msaada unaotolewa. Msanii pia anasisitiza suala la elimu katika kuondoa tatizo hili la ukoloni mamboleo. Elimu lazima ipatikane ili wananchi wapate kuzindua na kuona wapi wanaelekea. Kwa kufanya hivyo tuatalinda heshima ya taifa letu na kuepuka manyanyaso kutoka kwa wahisani na matokeo yake ni kujenga jamii mpya.

 (iv) Kupiga vita matabaka

Katika diwani hii, msanii anaonesha mivutano ya kitabaka iliyopo katika jamii yetu. Msanii ameonesha kuwa katika jamii yetu kuna matabaka mawili nayo ni tabaka tawala na tabaka la chini, yaani tabaka tawaliwa. Msanii anaendelea kuonesha kuwa, kuna uhasama mkubwa kati ya matabaka haya mawili, kwani tabaka tawala hukandamiza tabaka tawaliwa ambalo ni la wasionacho.

 Katika kuonesha msuguano huo wa kitabaka, msanii ametumia shairi la “Kansa” (uk.5)  kuonesha jinsi tatizo hilo lilivyo kubwa kama ugonjwa wa kansa, ambao huwa hauna uwezekano wa kupona. Matabaka katika jamii hayafai kwa kuigawa jamiii kulingana na hadhi na uwezo walionao, hivyo husababisha kundi moja kugandamizwa na kunyanyaswa kutokana na uwezo wao kuwa duni na kundi hili huwa ni la wale masikini wasio na chochote. Mawazo haya yanajadiliwa katika shairi la “Wasakatonge”(uk. 5) “Mvuja Jasho” na “Walala Hoi (uk.36) katika mashairi haya msanii ameonesha kuwa watu wa tabaka la chini, hufanya kazi kwa bidii zao zote katika shughuli zao ili kujikwamua na umasikini, lakini wanashindwa kwani malipo wayapatayo huwa duni sana ukilinganisha na uzito wa kazi zao.

Katika shairi la “Asali Lipotoja” (uk.37-38) anaonesha jinsi tabaka la juu linavyofaidika na matunda ya uhuru, wakati wale waliopigania uhuru huo ( tabaka la chini) hawafaidi matunda ya uhuru, wakati wale waliopigania uhuru huo ( tabaka la chini) hawafaidi matunda hayo. Vilevile shairi la “Kosa”(uk. 3) msanii anaonesha jinsi wananchi wanavyonyanyaswa na kugandamizwa na tabaka la juu kwa kunyimwa haki zao za msingi ambazo anastahili kupata.

 Katika shairi la “Hatuna Kauli” (uk. 8-9) msanii anaonesha jinsi nchi tajiri zinavyogandamiza nchi masikini na shairi la “Mumiani”(uk.34) anaonesha unyonyaji unaofanywa na watu na nyadhifa za juu katika nyanja mbalimbali za kimaisha kama vile mahakamani, watu hukoseshwa haki zao, hospitalini, vijijini wakulima hulipwa bei ndogo ya mazao yao licha ya yeye kutumia pesa nyingi katika kustawisha mazao hayo.

Utabaka katika jamii ni janga sugu lisiloweza kuepukika na unapomnyonya na mumnyima mtu haki, ipo siku utazinduka na kudai haki hiyo kwa nguvu kama anavyoonesha msanii katika shairi la “Hatukubali “ (uk. 38). Hapa msanii anaonesha jinsi watu wa tabaka la chini walivyochoshwa na kugandamizwa na kunyanyaswa na tabaka la juu, ijapokuwa inakuwa ni kosa kwao kufanya hivyo, kwani tabaka tawala hupenda kuwa juu zaidi milele na milele. Mawazo haya yanajitokeza pia katika shairi la “Marufuku”( uk.36)

 Hivyo msanii anaonesha kwamba kuwepo kwa matabaka katika jamii hukuwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini, kwani wanaofaidi maisha mazuri ni viongozi ambao ni tabaka tawala ( wasakatonge), ili kujenga jamii mpya lazima tupige vita matabaka.

 (v) kupiga vita unafiki na usaliti

 Suala la unafiki na usaliti linajitokeza kwa viongozi wa kisiasa na udini. Msanii anaonesha unafiki na usaliti katika mashairi ya ” Waso Dhambi” (uk.1) “Uasi” (uk.8) “Sikujua” (uk.28) “Nahaodha” ( uk.41-42) “Walamba Nyayo” ( uk.46-47), “Pepo Bila Kifo” (uk.14) na Madikteta (uk,21)

 Katika shairi la “Uasi” anaongelea unafiki na usaliti katika siasa na dini katika dini.Katika( uislam na ukristo) ambayo huwahubiria waumini wao kwa maneno makali yenye vitisho kwa kuwaonya waache uonevu wakati wao wenyewe maneno wayasemayo ni kinyume na matendo wayatendayo, vilevile katika dini, viongozi wanatenda matendo machafu kinyume na dini zao. Wakiwa mbele ya waumini wanajifanya hawatendi dhambi. Haya yanajidhihirisha wazi katika shairi la “Vinyonga” (uk. 49)

 Viongozi wa kisiasa wanaongea maneno mengi kwa wananchi na kuahidi vitu mbalimbali hata kama viko nje ya uwezo wao ili tu waonekane wanafaa. Wanapopata uongozi husahau na kufanya maovu kama vile ubadhirifu wa fedha na kula rushwa. Haya yameoneshwa wazi katika shairi la ” Vinyago” na Waramba Nyayo”(uk. 46-47). Tatizo hili linajitokeza tena katika shairi la ” Asali Lipotoja” hapa anaonesha jinsi watu walivyojitolea katika harakati za ukombozi wa nchi, lakini uhuru ulipopatikana nyadhifa zote za juu walishika wengine ambao hawakupigania uhuru huo na waliopigania wakaachwa na hali duni ya maisha.

 Kwa ujumla, unafiki na usaliti umejadiliwa sana katika diwani hii ya Wasakatonge na msanii anaoneshakuwa ili tuweze kujenga jamii mpya ni lazima tupige vita unafiki na usaliti wa viongozi wetu.

 (vi) Umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii

Msanii ameonesha umuhimu wa watu kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kujenga jamii mpya. Katika shairi la ” Klabu” ( uk. 50) msanii anawataka watu wote katika jamii kufanya kazi kwa bidii viwandani na mashambani ili kuleta maendeleo ya nchi kwa ujumla na kujenga jamii mpya.

 Vilevile katika shairi la ” Wanawake wa Afrika” (uk.2-3) anaeleza suala hilo la kufanya kazi kwa bidii kwa kuwashauri wanawake waamke toka usingizini na wachape kazi kwa bidii na wadai haki zao za msingi. Hivyo katika diwani hii, msanii anaonesha kuwa kufanyakazi kwa bidii kutaleta maendeleo ya nchi na hivyo kufanikisha kujenga jamii mpya.

 (vii) Kupiga vita mmomonyoko wa maadili

Katika diwani ya Wasakatonge msanii amejadili swala la mmonyoko wa maadili kulingana na wakati huu wa maendeleo ya sayansi na tekinolojia unaosababishwa na suala zima la utandawazi na kupeleka jamii kukosa mwelekeo wake uliokukwa mwema.

 Mfano amejadili suala zima la wanawake wenye tabia yaa kukutana kimwili wenyewe kwa wenyewe wakiwa jinsia moja “Wasagaji”. Amewaasa wanawake hao waachane nayo na watulie wapate wanaume wa kuwaoa na kufanya kama tendo hilo lilivyoruhusiwa kulingana na maadili ya kidini na ustaarabu wa jamii yetu na ameonesha hili katika shairi la ” Jiwe si Mchi” (uk. 18)

 Hakuishia hapo tu, pia amelijadili suala la umalaya, ambalo linawahusu wanawake wanaotembea hovyo na wanaume bila kuangalia hali mbaya iliyopo sasa katika jamii, hususani katika suala hili la ugonjwa wa UKIMWI linachongangiwa kiasi kikubwa na uasherati, hili ameelezea katika shairi la ” Wewe Jiko la Shamba” (uk. 44-48).

Limejadiliwa pia suala la mwenendo mbovu unaoikumba jamii yetu, mfano wa hilo ni katika shairi la “Unyama (uk.47-48) mshairi ameonesha masuala ya ubakaji na kunajisi yanavyofanywa na binadamu kama moja ya masuala yanayopelekea maadili kuporomoka.

 Hakuishia hapo, bali kuna suala zima la wanaume ambao wanatabia za kuingiliana kimwili wakiwa jinsia moja kwa mujibu wa wimbo wa “Taarab” uliokuwa ukiwazungumzia wanaume wa aina hiyo. Mshairi yeye,. Kwa kiasi Fulani ameonekana kuitetea tabia hii kwa kuelezea kuwa nao hupata raha zaidi wafanyavyo hivyo na wengine maumbile ndiyo huwaruhusu. Shairi la “Jawabu la Nahodha” (a( uk. 24-25). Kiuhalisia suala hili halipo kabisa katika mwenendo na maadili yetu ya Kitanzania. Ili tujenge jamii mpya lazima tupige vita mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu ambao ni kinyume na taratibu za jamii zetu.

 (viii) Kupiga vita hali ngumu ya maisha

 Hali ngumu ya maisha ni moja ya dhamira ambayo imejadiliwa na mwandishi Seif Khatibu amejadili jinsi watu wa tabaka la chini wanavyoishi katika shairi la “Walala Hoi” ( uk. 36) mshairi ameelezea jinsi hali duni ya maisha inavyowakabili makuli wa bandarini, wakulima, wavuvi na wachimba migodi, ameelezea jinsi gani kazi ngumu wanazofanya na malipo yao kuwa duni. Wanakubaliana na kazi za jinsi hii si kwa kupenda ila ni kutokana na ugumu wa maisha ambao umesababishwa na uongozi mbaya uliopo madarakani. Katika shairi “Mvuja Jasho” ( uk. 12-13) , mshairi anaonesha hali ya watu wa chini maisha yao yanavyokuwa duni, kipato chao ni kidogo ukilinganisha na mahitaji waliyonayo kwani kile wakipatacho hutumika kwa siku moja tu.

 Mshairi anaonesha jinsi hali ngumu ya maisha inavyolibadili bara la Afrika katika shairi la “Afrika” (uk. 6-8) mshairi anasema ni lini Afrika itakuwa kitalu cha shibe na sayari ya uzima. Hii inatuthibitishia kwamba bara la Afrika lipo katika hali mbaya ya maisha

 Seif Khatib anaelezea jinsi tabaka hili la chini mfano katika shairi la “Wasakatonge”, “Walala hoi”, wanavyotaabika na kukosa mwelekeo wa maisha na kuwa watu wa kkuhangaika katika shairi la “Twende Wapi” (uk. 20- 21).
Pia mshairi katika shairi la “Mama Ntiliye” anaonesha jinsi wanawake wanavyojitahidi kujishughulisha katika hali yao duni kwa kuuza vyakula japokuwa hawana mtaji mkubwa na nyenzo zao ni duni. Pia tukiangalia kiundani mshairi amejaribu kutumia lugha ya picha kuelezea suala hili, hapa amejaribu kumtumia Mama Ntiliye mwenye nyenzo duni kama jamii yenye hali duni lakini uduni wao haweza kusababishwa na majukumu na fitina wanaozitunga na kusababisha mtafaruku unaopelekea kutokuwa na maendeleo na matokeo yake maisha ni kuwa magumu.

 Na mwisho mshairi anaielimisha jamii, kuwa ni vizuri ukaanza kujikinga kuliko kusubiri tiba kwani tiba nyingine huweza isisaidie kama anavyosema katika shairi la “Tiba Isiyotibu” anaonesha madhara yanayopatikana kutokana na misaada inayotolewa na nchi hisani ili kuzisaidia nchi zinazoendelea. Misaada yao huwa ni ya kilaghai kwani huambatanishwa na masharti magumu yanayopelekea hali ngumu ya maisha katika nchi kuzidi kuwa mbaya.  Hivyo basi, si misaada yote huweza kuwa suluhisho la tatizo la hali mbaya ya maisha katika nchi bali huweza kuleta ugumu zaidi ya awali. Hivyo, ili tujenge jamii mpya ni lazima tupige vita hali ngumu ya maisha.

Ukombozi
Ukombozi ni dhamira nyingine kuu anayoijadili msanii katika diwani hii ya Wasakatonge. Katika diwani hii, amejadili kwa kiasi kikubwa ukombozi wa wanajamii dhidi ya unyonyaji, uonevu na ugandamizwaji wa aina yoyote ile. Katika kujadili dhamira hii, msanii ameonesha ukombozi wa kisiasa kiutamaduni, kiuchumi na kifikra( kimawazo).

 Katika Ukombozi wa Kisiasa msanii anaonesha kuwa uhuru ni njia mojawapo ya kujitoa katika utawala wa kikoloni. Katika shairi la “Afrika” (uk.6-8) msanii anaonesha umuhimu wa nchi za Kiafrika kujikomboa kutoka mikononi mwa wakoloni ili kujiletea maendeleo. Katika shairi la “Nuru ya Tumaini” (uk. 9-10) anaonesha nchi inavyokuwa baada yakujikomboa na analinganisha ukombozi sawa na  alfajiri njema. Katika ukombozi wa kisiasa, msanii anawataka Waafrika waondoe ukoloni na vilevile wawaondoe viongozi wabovu na madikteta.

Katika Ukombozi wa Kiutamaduni, msanii kwa kiasi kikubwa anazungumza juu ya ukombozi wa mwanamke. Msanii anawataka wanawake wajikomboe kutoka katika lindi la uonevu na unyanyaswaji wa kijinsia, kwani wanaonekana ni viumbe dhaifu wasio na mchango wowote katika jamii,  haya yanaoneshwa wazi katika shairi la “Wanawake wa Afrika” (uk.16).

Katika kujadili suala la ukombozi wa mwanamke, msanii ameonesha kuwa ili waweze kujikomboa lazima wapate elimu na kuzitambua haki zao za msingi. Pia lazima waungane na kuwa kitu kimoja na waachane na mambo ya kifitina baina yao ili waweze kufanikiwa katika harakati zao za kujikomboa. Haya yanaoneshwa katika shairi la ” Wanawake wa Afrika” ( uk. 16).

 Vile vile katika shairi la ” Mama Ntiliye” ( uk. 17-18) msanii anaonesha kuwa ili wanawake wajikomboe kiuchumi lazima wafanyakazi kwa bidii. Msanii anaonesha kuwa mwanamke badala ya kupiga majungu wajibidiishe katika kazi ili waweze kujikomboa kiuchumi.

 Katika shairi la “Tohara” (uk.2) msanii anaitaka jamii kuachana na mila potofu za kuendeleza tohara kwa wanawake ambazo huleta matatizo kwa wanawake sehemu zao za siri, kwa mfano kupata vidonda ambavyo huwapelekea kupata maradhi ya Pepopunda na “UKIMWI” Pale wanapochangia vifaa vya kutahiria. Msanii anataka jamii iachane na tohara kwa wanawake kwa kuwataka wanajamii kuipiga vita ili kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.

 Kuhusu Ukombozi wa Kiuchumi, msanii anawataka wanajamii waungane na kufanyakazi kwa bidii ili kuondoa umaskini katika nchi yetu. Anataka wanajamii waoneshe juhudi katika kazi mbalimbali viwandani, shambani nk. ili kuinua uchumi wa nchi na kuondokana na umasikini.Haya yanajionesha wazi katika shairi la “Walala Hoi, Wasakatonge, Mvuja Jasho, Mama Ntiliye, Wanawake wa Afrika” n.k

Ukombozi wa Kifikra
unajitokeza katika shairi la “Wanawake wa Afrika” ambapo msanii anawataka wanawake wapewe elimu ili waweze kuzifahamu haki zao na hivyo kuacha kugandamizwa na kunyanyaswa kama wanavyofanyiwa na wanaume.

Dhamira dogondogo


i. Mapenzi
Mshairi amelijadili mno suala la mapenzi katika maisha. Mwandishi ameeleza mapenzi kama kitu chenye kuwafanya wawili wapendanao kusahau karaha zote za dunia ikiwa watapendana kidhati kwani mapenzi yao yatanoga na kuzaa faraja mioyoni mwano kama mshairi anayofafanua katika shairi la ” Yeye na Mimi” (uk.36. ). Si hivyo tu bali msanii amezidi kuelezea juu ya suala hili katika shairi la “Mahaba” (uk.1) ambapo ameelezea kuwa unapokuwa katika mapenzi huweza kufanya lolote lile ili kulinda penzi, pia penzi huweza kumfanya mtu kuwa tayari kujitoa mhanga au kuonekana na wazimu pale anapokolea kisawasawa.


Pia mshairi anazidi kuelezea kwa kuonesha jinsi penzi linavyoweza kuwa adhabu pale mtu mmoja anapomsaliti mwenziwe ama anapofariki na kumwacha mwenziwe akihangaika au hatakuathirika kiafya haya yameonyeshwa katika shairi la “Usiku wa Kiza” (uk. 27)

 Licha ya hiyo, mtunzi amwewatahadharisha watu kuwa makini katika mapenzi. mfano katika shairi la “Sitakujua” (uk. 28) ambapo anamuelezea yule mtu ambaye anajuta, baada ya kumpata yle asiyemtaka maishani mwake. Na pia anataka tusiwe na pupa katika suala la mapenzi kama anavyoeleza katika shairi la ” Nilichelewa Kupendwa” (uk. 27)

Licha ya hiyo, mtunzi amewatahadharisha watu kuwa makini katika mapenzi mfano katika shairi la “sitakujua” ( uk.28) ambapo anamuelezea Yule mtu ambaye anajuta, baaada ya kumpata yule asiyemtaka maishani mwake. Na pia anataka tusiwe na pupa katika suala la mapenzi kama anavyoeleza katika shairi la “nilichelewa kupendwa” (uk. 41)

 
Mshairi amejadili mapenzi kulingana na wakati hu wa sasa. Katika wakati huu, mapenzi yamekuwa kama bidhaa sokoni ambapo unapokuwa na pesa au hali nzuri ya maisha ndipo utapa penzi, lakini kinyume na hapo utabakia na sononeko la moyo kwa kupewa ahadi zisizo za kweli na mfadhaiko wa moyo hata kujiona kutokuwa na muhimu duniani kama ilivyoonyeshwa katika shairi la ” Nilikesha” ( uk. 23-24).

Hivyo ni dhahiri kuwa katika hali tuliyonayo sasa na kulingana na na maelezo ya mashairi, ni vigumu kupatikana kwa upendo wa dhati. Maelezo hayo ameyatoa katika shairi la “Pendo Tamu” (uk.25) kitikio anaelezea ni vigumu kulipata lililotamu lenye maelewano lililoisha na lenye raha katika dunia kama hii.
Katika kuonesha mapenzi mshairi, kiasi kikubwa amejielezea mapenzi analiyonayo kati yake na Yule ampendaye, wanavyopendana kwelikweli mfano katika shairi la “Nilinde” (uk.15), “Yeye na Mimi” (uk.39,) “Pendo Tamu”(uk. 35), “Tutabaki Wawili” (uk.26) yote hayo yanaonesha upendo wa dhati kwa wawili wapendanao. Ni vizuri umpendapo mtu ukamweleza ukweli Kama mshairi katika shairi la “Kauli Yako” (uk.27), akimsihi mpenzi wake amdhibitishie kutoka ndani ya moyo wake kama kweli anampenda.

Pia Ni vizuri unapokuwa umempata mpenzi ukawa na heshima na ustarabu baina yenu na si vizuri kupuuzia, mara nyingine inaweza kusababisha mtafaruku baina yenu mfano katika shairi la “Si Wewe” (uk.21). Na unapojua mpenzi wako anakupenda kwa dhati basi ni vizuri ukazienzi hisia zake. Si vizuri ukamdhihaki kwa kuchezea upendo alionao kwako kama anavyosema katika shairi la”Wewe Wajua” (uk.29.) Na si kumkosesha mtu mwelekeo wake wa maisha, mfano wa hilo ni katika shairi la “Machozi ya Dhiki” (uk. 28), msahiri anaelezea jinsi dhuluma ya mapenzi inavyoweza kumtesa mtu na kumsababishia maumivu mithili ya kisicho na dawa.

 (ii) Nafasi ya mwanamke katika jamii.
Mshairi amemchora mwanamke kama kiumbe dhaifu asiyeweza kujitetea dhidi ya mila potofu zinazomkandamiza na kumuumiza. Mwandishi amelionesha suala hili kama ifuatavyo;
 
Ameonesha jinsi mila na tamaduni ambazo humuathiri mwanamke kama inavyooneshwa katika shairi la “Tohara” (uk. 2). khatib anonesha jinsi wanawake wanavyoathirika na suala hili la tohara kwa kuonesha athari wazipatazo kama kuambukizwa magonjwa mfano UKIMWI. Kutokana na kutumia chombo kimoja wakati wa kutahiriwa/ kukeketwa, kuharibika sehemu za siri, kupatwa na shida wakati wa kujifungua ambapo hupata maumivu makali kupita kiasi.
 
Vilevile ameoneshwa mwanamke kama mtu fitini asiyependa maendeleo. Hutumia muda wake mwingi katika kuchonganisha watu kwa kupika uongo kuusambaza na ametumia taswira ya shairi la “Mama Ntiliye” (uk.17-18) kufikisha maudhui haya na hakuishia hapo tu bali amewaasa wanawake kuacha tabia hiyo mbaya kwani za mwizi ni arobaini na ipo siku watakuja kuadhirika watakapokamatwa na watu wenye kukerwa na tabia zao.
 
Mwanamke amechorwa kama chombo cha kazi. Katika jamii nyingi hasa za kiafrika mwanamke huwa ndiye mfanyashughuli zote za nyumbani na hata zile za shambani. Licha ya majukumu hayo pia, mwanamke ndio mlezi wa familia kama inavyoelezwa katika shairi la “Mwanamke” (uk.16).

Pia mwanamke amechorwa kama chombo cha starehe, ameonyeshwa kama chombo cha kuliwaza/ kuburudisha wanaume pale watokapo katika shughuli zao. Na pia huwa hana thamani katika jamii yake kama inavyoelezwa katika shairi hilohilo la “Mwanamke”.

Mshairi amemweleza mwanamke kama kiumbe asiye na maadili katika shairi la ” Wewe Jiko la Shamba” (uk. 44) ambapo amemwonesha mwanamke kama mtu Malaya, ambaye hutembea hovyo na wanaume bila kuangalia madhara yake ambayo huwa ni magonjwa ya zinaa, hasa tatizo kubwa la ugonjwa wa UKIMWI ambao hauna tiba. Mshairi anaelezea zaidi katika shairi la “Vitamu” (uk.44) kwa wale wenye tabia mbaya kama hizo waache kwani wanaume huvutiwa mno na wanawake waliolelewa kutunzwa kwa maadili mema, ambao ndio hasa wanaume huwakimbilia nah hivyo basi ni vizuri mtu kujiheshimu ili kulinda hadhi yako.

Mwisho, mshairi anawasa zaidi na kuwashauri wanawake wote wa Afrika kwa ujumla, kwa kuwapa njia mbadala za kuweza kujukwamua dhidi ya matatizo yanayowakabili. Amewaonesha njia za kufuata ambazo ni kuungana, kushirikiana na wajitahidi katika suala zima la taaluma / elimu ili wajielimishe na kuweza kuzitetea kwa umoja haki zao bila kubaguana na kuachana na mambo ya umbea , majungu na fitina; vitu ambavyo vitarudisha nyuma katika harakati za kukwamua, katika shairi la “Wanawake wa Afrika” (uk10-11).

Ujumbe

  • Ukiteta ni kikwazo kikubwa cha maendeleo. Jamii haina budi kung’oa utawala wa kidikteta katika jamii zao.
  • Mapenzi ya dhati katika jamii ni suala la muhimu katika jamii.
  • Heshima kwa jinsia zote ni muhimu kuzingatiwa ili kuletea usawa wa kijinsia katika jamii.
  • Ukoloni mamboleo  na aina zote za unyonyaji ni lazima zipigwe vita katika ujenzi wa jamii mpya

edu.uptymez.com

Falsafa

Mwandishi anelekea kuamini kuwa jamii yoyote haiwezi kuendelea kama hakuna usawa katika jamii husika.

 Msimamo wa mwandishi

 Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi. Mwandishi ameweza kuonesha matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii bila woga. Mwandishi pia amependekeza mbinu za kuondokana na matatizo hayo. Miongoni mwa matatizo yanayotajwa na mwandishi kuwa ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya ni haya.

  • Uongozi mbaya.
  • Matabaka
  • Unafiki
  • Dhuluma
  • Unyonyaji

edu.uptymez.com

FANI
Mwandishi ametumia miundo ya aina mbalimbali. Anaweza kutumia muundo wa tarbia, tathlitha na sabilia. Mifano ya mashairi na aina ya miundo iliyotumika ni kama ifuatavyo.

 (i) Sabilia: Huu ni muundo unaohusisha mashairi yenye mistari mitano na zaidi. Mfano wa mashairi yenye muundo wa Sabitia ni “Kosa” (uk.3), “Nilikesha” (uk.23), “Walala Hoi” (uk.36 -37), “Nahodha” (uk. 41 -42) na “Unyama” (uk.47)

 (ii) Tarbia: Huu ni muundo unaohusu mashairi yanayoundwa na ubeti wenye mistari mine (4) tu. Mfano wa mashairi yenye muundo wa tarbia ni “Mcheza
Hawi Kiwete” (uk.32) “Siwi Maji Mafu” (uk.33), na “Pendo Tamu” (uk.35).

 (iii) Tathilitha : Huu ni muundo unaohusu mashairi yanayoundwa na mistari mitatu (3) katika kila ubeti: Mfano wa mashairi hayo ni “Hatuna Kauli” (uk.8), “Sikujua” (uk.28) na “Kansa” (uk 4).

Mtindo :
Mshairi ametuamia mtindo wa aina mbili;

  1. Mtindo wa kimapokeo unaofuata urari, vina na mizani. Mfano wa mashairi yanayofuata mtindo wa kimapokeo :

     (i) Buzi Lisilochunika (uk27)

    (ii) Wewe Jiko la Shamba (uk.27)

    (iii) Siwi Maji Mafu ( uk 33)

    (iv) Mcheza hawi Kiwete (uk 32)

  2. Mtindo huria (mavue) ni mtindo ambao haufungwi na kanuni za urari wa vina na mizani

    (i) Si wewe (uk.21)

    (ii) Sikuliwa Sikuzama (uk.22)

    (iii) Miamba (uk.29)

    (iv) Marufuku (uk.36)

    (v) Vinyago (uk. 49)

edu.uptymez.com

Hata hivyo, mashairi mengi ni yale ya kisasa ambayo hayafuati urari wa vina na mizani.

Matumizi ya lugha

Wasakatonge ni diwani ambayo imeandikwa kwa kutumia lugha inayoeleweka kwa wasomaji wa diwani hii. Imeshehenezwa kwa tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.

Tamathali za semi

Tashihisa. Hii ni tamathali ya semi yenye kuvipa vitu uwezo wa kutenda kama binadamu.

 Kwa mfano:

  • Radi yenye chereko” katika shaiti la “Afrika”
  • Pendo lenye tabasamu” katika shairi la “Pendo Tamu”
  • Inaumwa Afrika” Katika shairi la “Tiba isiyotibu”
  • Kazi kikajitajirisha” katika shairi la “Twende wapi”

edu.uptymez.com

Sitiari : Hii ni tamathali ya mlinganisho. Vitu viwili hulinganishwa moja kwa moja bila kutumia viunganishi vya mlinganisho.

  • Ndwele ni maskini” katika shairi la “Tiba isiyotibu.
  • Uchoyo ni sumu” katika shairi la “Pendo tamu”
  • Mate si baragumu” katika shairi la “Mtemea mate mbinguni”

edu.uptymez.com

Tashibiha : Hii ni tamathali ya mlinganisho wa vitu viwili tofauti kwa kutumai viunganishi kama vile; kama, mfano wa, mithili ya, sawa na, n.k.

Kwa mfano:

  • Lanuka kama ng’onda” katika shairi la “Kansa”
  • Hubakia kama wanga” katika shairi la ” Nilichelewa kupendwa”

edu.uptymez.com

 Mbinu Nyingine za Kisanaa.

Takriri : Hii ni mbinu ya kurudiarudia tungo. Katika diwani hi mbinu hii imejitokeza katika mashairi yafuatayo:

  • Buzi lisilochunika” mshairi anasema  Hili buzi, buzi gani lisiloelimika

edu.uptymez.com

Neno “buzi” limejirudiarudia katika mstari mzima.

Takriri nyingine zimejitokeza uk 4 mshairi anaposema, jamii imeoza imeoza ya nuka” (neno oza) uchafu wachomoza, wachomoza, wafuka. (Neno chomoza).

Ujenzi wa picha na taswira

Mashairi ametumia yugha ya picha kueleza hisia zake baadhi ya taswira hizo ni pamoja na hizi zifuatazo

i. Nahodha: imetumika kueleza kiongozi

ii. Jahazi : imetumika kueleza nchi

iii. Jiwe si mchi: imetumika kueleza wanawake wasagaji

iv. Tonge la ugali: uchu wa madaraka

vi. Vinyago: wasaliti

Jina la Kitabu

Jina la kitabu Wasakatonge linasadifu yale yanaelezwa ndani ya kitabu. Wasakatonge ni watu ambao wanapigania maisha yao ili kupata chakula chao cha kila siku (watu maskini). Jina la kitabu linasadifu yaliyomo ndani kwa sababu mashairi mengi yaneleza matatizo wanayokumbuna nayo watu wa tabaka la chini.

Vilevile kuna shairi pia ndani ya kitabu hiki ambalo ameliita “Wasakatonge” ambapo mshairi anaeleza fani na maudhui ya mashairi yake kuwa yatahusu Wasakatonge.

Hivyo basi Wasakatonge kama jina la kitabu linasadifu yaliyo ndani ya kitabu kama ambavyo imeelezwa hapo juu kuwa mashairi mengi yanazungumzia matatizo ya watu wa tabaka la chini na pia kuna shairi la Wasakatonge ndani ya kitabu hiki.

KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI

Kufaulu

Mwandishi amefaulu kimudhui kwani amewaza kueleza matatizo sugu yanayoigusa jamii yake na kuweza kuonesha mbinu mbalimbali za kuondokana na matatizo hayo.

Mwandishi ameweza kuonesha ufundi wake katika kuandika mashairi mengi kwa kutumia mitindo yote, miundo ya ushairi mbalimbali na lugha iliyojaa lugha za picha (taswira) tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.

Kutofaulu

Mwandishi ameshindwa kutumia Kiswahili sanifu na badala yake lahaja ya Kiunguja imetawala sana katika mashairi yake. Hili ni tatizo kwani wasomaji wengi wanaweza wasiwe na ujuzi wa kuelewa lahaja mbalimbali.

Share this post on: